Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda (katikati), akiwa na Wajumbe wa Kamaati ya Ulinzi na Usalama wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Igoma iliyofaanyika Februari 01, 2026. ............................... Na Mwandishi Wetu, Mbeya |
Kituo hicho hadi kukamilika kwake kimegharimu Sh. Milioni 150.
Ujenzi wa kituo hicho ni mkakati wa serikali kuimarisha ulinzi, usalama, na kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliokwenda sambamba na makabidhiano ya miundombinu hiyo, Mhe. Itunda amesema ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha mazingira ya kazi ya vyombo vya ulinzi nchini.
Mhe. Itunda amebainisha kuwa uwekezaji huo mkubwa katika sekta ya usalama unalenga kudumisha amani na utulivu, mambo ambayo ni nguzo kuu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ndani ya Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Alisema serikali haitafanya muhali kwa yeyote atakayebainika kukiuka haki za wengine na amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya dola.
Aidha, Mhe. Itunda amewataka wakazi wa Igoma na maeneo jirani kukitunza kituo hicho kipya na kuona miundombinu hiyo kama mali yao, ili iweze kudumu na kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya polisi na jamii (Polisi Jamii) ndiyo silaha pekee ya kutokomeza uhalifu.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi, akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP),Benjamin Kuzaga, pamoja na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mbalizi ambao kwa pamoja wameahidi kuongeza ufanisi wa kazi kutokana na kupatikana kwa kituo hicho kipya.













No comments:
Post a Comment