𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐊𝐔𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐇𝐔𝐃𝐔𝐌𝐀 𝐙𝐀 𝐖𝐀𝐙𝐄𝐄 𝐍𝐀 𝐅𝐔𝐑𝐒𝐀 𝐙𝐀 𝐊𝐈𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈 𝐊𝐖𝐀 𝐕𝐈𝐉𝐀𝐍𝐀 – 𝐌𝐀𝐇𝐔𝐍𝐃𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, May 31, 2026

𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐊𝐔𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐇𝐔𝐃𝐔𝐌𝐀 𝐙𝐀 𝐖𝐀𝐙𝐄𝐄 𝐍𝐀 𝐅𝐔𝐑𝐒𝐀 𝐙𝐀 𝐊𝐈𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈 𝐊𝐖𝐀 𝐕𝐈𝐉𝐀𝐍𝐀 – 𝐌𝐀𝐇𝐔𝐍𝐃𝐈

Na Jackline Minja- WMJWM Dodoma

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali itaendelea kuweka kipaumbele katika ustawi wa wazee na uwezeshaji wa vijana kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha yao na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Mhe. Mahundi ameyasema hayo tarehe 30 Mei, 2026 wakati akizungumza na wageni kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Maryprisca Women Foundation wakiongozana na Machifu kutoka Mkoa wa Mbeya waliowasili mkoani Dodoma kwa ziara ya mafunzo na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika Mji wa Serikali Mtumba pamoja na shughuli zinazotekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha wazee wanapata huduma stahiki ikiwemo bima ya afya na kuishi katika mazingira salama na bora, huku ikiimarisha mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia fursa za mikopo, mafunzo ya ujasiriamali na programu mbalimbali za maendeleo.

Katika ziara hiyo, wageni hao walipata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na kujionea majengo ya kisasa ya Wizara na Taasisi mbalimbali yaliyojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mMhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua ambayo imeendelea kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.

Aidha, walijifunza kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na Wizara katika kuimarisha ustawi wa jamii, hususan kwa makundi maalum yakiwemo wazee, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wao, baadhi ya machifu walioshiriki ziara hiyo wameipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba na kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika masuala ya maendeleo ya jamii.

Pia wamempongeza Mhe. Mahundi kwa juhudi zake katika kusimamia utekelezaji wa mipango inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, hususan makundi maalum.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad