𝐖𝐀𝐋𝐈𝐌𝐔 𝐖𝐀𝐋𝐈𝐀 𝐑𝐀𝐅𝐔 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐓𝐎𝐀 𝐂𝐖𝐓 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐔𝐍𝐆𝐀 𝐂𝐇𝐀𝐊𝐀𝐌𝐖𝐀𝐓𝐀 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, June 16, 2026

𝐖𝐀𝐋𝐈𝐌𝐔 𝐖𝐀𝐋𝐈𝐀 𝐑𝐀𝐅𝐔 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐓𝐎𝐀 𝐂𝐖𝐓 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐔𝐍𝐆𝐀 𝐂𝐇𝐀𝐊𝐀𝐌𝐖𝐀𝐓𝐀

Wakurugenzi, maafisa utumishi watajwa.
Muonekano wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Singida
................................................

WALIMU Wanachama wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) wamelalamikia kitendo cha baadhi ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wanaohamia kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuzuiwa kujiunga na chama hicho ambacho kipo kwa mujibu wa sheria.


Wanaotuhumiwa kuwazuia walimu hao ni Wakurugenzi, Maafisa Utumishi Wakuu na Maafisa Utumishi Wasaidizi wa Halmashauri mbalimbali nchini.


Walimu hao wanadai kuwa licha ya kujiunga na CHAKAMWATA kwa kufuata hatua zote za kisheria, Maafisa hao wanaoingia kwenye mfumo wa mishahara yao (LAWSON) na wamekuwa wakikataa kuwaunga CHAKAMWATA walikojiunga badala yake wanawalazimisha wabaki CWT walikojitoa.


Maafisa hao wanadaiwa kukataa kuondoa makato ya 2% ya CWT na kuingiza michango ya 1% ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya Walimu wanaojitoa kutoka CWT na kujiunga na CHAKAMWATA.


Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwepo kwa hali hiyo ya kuzuiwa kwa Walimu kujiunga na vyama vingine walivyovichagua kwa hiari yao na hali hii ni kubwa na iko karibu nchi nzima.Muonekano wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

...........................................

Mwandishi alifanikiwa kuwasiliana na Wakurugenzi Watendaji wa baadhi ya Halmashauri za Wilaya, Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Miji, Maafisa Utumishi Wakuu na Wasaidizi pamoja na baadhi ya Wanasheria wa Serikali wa Halmashauri za Wilaya ili kujua wanasema nini kuhusu malalamiko ya Walimu dhidi yao.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Justice Kijazi ambaye analalamikiwa na walimu hao kuwa anakataa kutekeleza maagizo ya kuondoa makato ya 2% ya CWT na kuingiza michango ya 1% ya CHAKAMWATA kwenye mishahara yao alipopigiwa simu kujibu madai hayo alisema asingeweza kusema lolote kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.


Hata hivyo, alimueleza mwandishi wetu kwamba angempatia namba ya simu ya afisa aliyemuachia ofisi kwa wakati huo, lakini hakufanya hivyo. Alipopigiwa tena kukumbushiwa hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (meseji) hakujibu. 

Hata hivyo malalamiko ya Walimu katika jiji hilo  yapo kuanzia Mwezi Machi 2025, muda ambao Mkurugenzi Justice Kijazi amekuwepo ofisini.


 Walimu wapatao 881 wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wanamlalamikia Mkurugenzi wao kuwa ameyashikilia majina yao kwa zaidi ya mwaka mmoja na mkurugenzi huyo amewazuia wasiondolewe CWT wala wasiingizwe CHAKAMWATA tangu mwaka 2025 licha ya walimu hao kukamilisha taratibu zote zinazohitajika kisheria.


Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wanamlalamikia Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Afisa Utumishi Mkuu pamoja na Afisa Utumishi Mkuu Msaidizi kwa kukataa kutekeleza maelekezo yao ya kuondoa makato ya 2% ya CWT na kuingiza michango ya 1% ya CHAKAMWATA kwenye mishahara yao baada ya kukamilisha hatua zote za kisheria.


Mwandishi wetu alifanikiwa kupata barua ya mmoja wa walimu waliokataliwa kuhamishwa kutoka CWT kwenda CHAKAMWATA.


Barua hiyo iliyosainiwa na Fatuma Mabira yenye kumbukumbu namba TDC/PF. 1541/119 ya tarehe 05/11/2025, akimjibu Mwalimu Shabani Ahmadi Napachihi wa Shule ya Msingi Mji Mpya kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amekataa kumwondoa Mwalimu huyo kutoka CWT alikojitoa na kumpeleka CHAKAMWATA alikojiunga kwa hiari yake na kwamba kwenye Wilaya yake ya Tandahimba Chama halali cha Walimu ni CWT tu na kwamba Mwalimu huyo ataendelea kukatwa 2% za CWT kwa lazima (ndivyo inavyosema sehemu ya barua hiyo). 


 Mwandishi wetu alipomtafuta kwa simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mariam Mwanzalima hakuweza kupatikana, licha ya kupigiwa mara kadhaa.


Wakati Mabira akimtaka mwandishi wetu awasiliane na Mwanzalima kwa ajili ya kupata ufafanuzi kuhusu madai hayo alifanikiwa kupata nakala ya barua nyingine iliyosainiwa na kiongozi huyo.


 Barua hiyo yenye kumbukumbu namba J. A. 25/414/02/30 ya tarehe 16 Juni 2025 ilikuwa ikimjibu Mwenyekiti wa CHAKAMWATA wa wilaya hiyo kuwa amekataa kuwaondoa CWT na kufuta makato ya 2% ya CWT kwenye mishahara ya Walimu wote waliohama CWT na kujiunga na CHAKAMWATA na kwamba amekataa kuingiza michango ya 1% ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya walimu hao.

Muonekano wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Madaba Songea mkoani Ruvuma.

........................................  

Madai ya Mkurugenzi huyo kuhusu msimamo wake kwa mujibu wa barua hiyo ya Mwenyekiti wa CHAKAMWATA wa Wilaya ya Tandahimba ni kuwa hayo ni maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kupitia Waraka namba 1/2022 wa Msajili wenye kumbukumbu namba DA. 76/380/01/67 wa tarehe 07 Juni 2022, kuwa CHAKAMWATA hakina sifa za kufanyakazi katika Halmashauri ya  Wilaya ya Tandahimba.


Madai ya Mkurugenzi huyo yanafanana na madai ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dk. Fredrick Sagamiko ambaye kupitia barua yenye kumbukumbu namba HA. 27/294/02/02 ya tarehe 19 Mei 2025, akimjibu Mratibu wa CHAKAMWATA Mkoa wa Dodoma.


Katika barua hiyo mkurugenzi huyo alikataa kuondoa makato ya 2% ya CWT ili kuingiza michango ya 1% ya CHAKAMWATA kwenye mishahara ya Walimu 78 waliokuwa wamejitoa kutoka CWT na kujiunga CHAKAMWATA.


Mkurugenzi huyo kwenye barua yake anasema hayo ni maagizo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini kupitia Waraka wa Msajili namba 1/2022.


Taarifa zaidi zinasema kuwa unaodaiwa kuwa ni Waraka wa Msajili namba 1/2022 uliandikwa kwenda kwa Makatibu wakuu wa Vyama vya Wafanyakazi na wala siyo kwenda kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya.


Hata hivyo, zipo taarifa kuwa waraka huo  unaodaiwa kutolewa na Msajili unapingana na Sheria ya vyama vya Wafanyakazi na inadaiwa ulilenga kukibeba Chama cha Walimu Tanzania (CWT) dhidi ya CHAKAMWATA na sasa unatumika vibaya na wakurugenzi wa halmashauri kuwazuia walimu wote nchini wasijiunge CHAKAMWATA.


Aidha, kuna madai kuwa Msajili huyo wa vyama vya Wafanyakazi aliwahi kukipiga marufuku CHAKAMWATA na baadaye akakifuta kutoka kwenye rejista ya Vyama vya Wafanyakazi nchini wakati anajua fika kuwa Sheria haimpi mamlaka ya moja kwa moja kufanya hivyo dhidi ya Vyama vya Wafanyakazi.


 Baadaye Msajili alifungua  kesi namba 13 ya mwaka 2022 ya kutaka  CHAKAMWATA ifutwe ambapo ilifutwa.


CHAKAMWATA ilipingana na uamuzi huo hivyo, ilikata rufaa katika kesi namba 170 ya mwaka 2023 na hatimaye ikashinda na kurejeshewa usajili wake na Mahakama ya Rufani Februari 27, 2025.


Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro madai yaliyotolewa na walimu waliohamia CHAKAMWATA yanafanana na madai ya Halmashauri nyingine ya kuzuiwa kujitoa CWT ambapo walimu 200 wamezuiwa.

Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya

..................................

Mwanasheria wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Elikarim Tyeah alipoulizwa kuhusu malalamiko ya Walimu hao alikataa kusema chochote kwa madai kuwa msemaji wa jambo hilo ni Mkurugenzi.


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Saida Mahugu alipopigiwa, simu yake ilikuwa ikiita  bila ya kupokelewa.


Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli alipopigiwa simu na mwandishi wetu  kuhusu madai ya walimu waliotaka kujiunga CHAKAMWATA kuzuiwa kuondoka CWT na kuwa tangu mwezi Julai 2025 mpaka mwezi Machi 2026, zaidi ya Walimu 130 makato yao ya 1% bado hayajaingizwa,  alisema hakuwa na taarifa hiyo.


Alisema mara atakaporudi kutoka safari Jijini Dodoma atalifanyia kazi jambo hilo na kila mwalimu atapewa haki yake.


Aidha, alisema alikwishaagiza walimu wasiingiliwe kwenye uhuru wao wa kuchagua ni chama gani cha Walimu wanachotaka kujiunga nacho.


Hata hivyo mpaka tunapoandika habari hii, Mkurugezi huyo hajayafanyia kazi madai hayo.


Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi walimu waliohamia CHAKAMWATA wamekuwa na malalamiko ya kuzuiwa kutoka CWT,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Abdallah Nandonde alipogigiwa simu kwa lengo la kupata ufafanuzi wa suala hilo, simu iliita bila kupokelewa.


Afisa Utumishi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Salum Kalyomunda alipopigiwa na kuulizwa kuhusu malalamiko ya Walimu zaidi ya 300 wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambao amewazuia kujitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA tangu mwezi Machi 2025, alisema yuko kwenye kikao, akitoka atapiga lakini tangu siku hiyo kila alipopigiwa simu hakupokea.


Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, inadaiwa walimu zaidi ya 250 waliojitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA wamezuiwa, alipogiwa simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo   Erica Yegella ili kuzungumzia suala hilo simu yake iliita mara kadhaa bila ya kupokelewa.


 Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza inadaiwa Walimu zaidi ya 170 wamezuiliwa kujitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Amon Mkoga, alipopigiwa simu alisema anawaomba viongozi wa CHAKAMWATA waende ofisini kwake wakazungumze.


 Uchunguzi wetu umebaini kuwa Viongozi wa CHAKAMWATA walipokwenda, Mkurugenzi huyo aliwakabidhi kwa Afisa Utumishi ambaye anadaiwa kuwazuia walimu hao tangu mwaka 2025, na hakuna utekelezaji wowote uliofanyika mpaka tunapotoa habari hii.


Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, alipopgiwa simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Elizabeth Gumbo na kuelezwa madai ya Maafisa Utumishi kuitisha kikao cha viongozi na wanachama wa CHAKAMWATA kwa siku mbili tofauti ambapo pamoja na kuwapa vitisho, maafisa hao wakiongozwa na Afisa Mkuu Iddi Kalungonji, waliwaambia walimu hao hawatawatoa CWT na kuwaingiza CHAKAMWATA mpaka watakapohojiwa na Idara ya Utumishi kuhusu kujitoa kwao.


 Mkurugenzi huyo alisema hakuwa na taarifa hiyo na hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka atakapo maliza likizo yake.Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nyag’wale mkoani Geita

................................................

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, alipopigiwa simu Afisa Utumishi Samina Gullam na kuulizwa kuhusu kuwazuia walimu zaidi ya 217 waliojitoa CWT na kujiunga na CHAKAMWATA tangu 2025, alijibu kuwa hawezi kuzungumza chochote mpaka mwandishi wetu aende ofisi kwake.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, baada ya kuulizwa kama anajua kuna walimu 48 ambao wamejitoa CWT na wanataka kujiunga na CHAKAMWAKA lakini hawapewi ushirikiano tangu Machi 2026 wakati kisheria wanapaswa kutekelezewa matakwa yao ndani ya siku 30 tu.


Mkurugenzi huyo alisema hajui chochote na kueleza kuwa ni haki ya walimu kujiunga na chama chochote anachokitaka lakini kuna taratibu ambazo wanapaswa kuzifuata.


Hata hivyo walimu hao walidai kuwa taratibu hizo tayari walishazifuata ikiwa ni kujaza fomu namba 15 kutoa notisi kwa CWT na kwa mwajiri.


Katika Wilaya ya Singida DC Walimu waliohamia CHAKAMWATA kutoka CWT walilalamikia kuzuiwa na Afisa Utumishi wa wilaya hiyo Edwin Mwampamba kwa madai wanasubiri kupata barua  kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.


Mwampamba alipopigiwa simu na mwandishi wetu ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo alikataa kusema chochote kwa kuwa msemaji ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,


Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Stella Chaula alipopigiwa simu ili kutoa ufafanuzi alisema hajui kuhusu madai hayo na kuwa yupo safarini nje ya Mkoa wa Singida pindi atakaporudi atafuatilia jambo hilo.


Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya Florah Luhala walimu wanamlalamikia kama wilaya zingine ambapo Septemba 26, 2025 aliitisha kikao cha Vyama vya Walimu nje ya CWT kwa nia ya kuvipiga marufuku ambapo Katibu Mkuu wa CHAKAMATWA ambaye alihudhuria kikao hicho pasipo kutarajiwa alimpinga.


Luhala alipopigiwa simu na mwandishi wetu ili kuzungumzia suala hilo, alisema hakuna mwalimu ambaye anazuiwa kujiunga na chama kingine inachotakiwa ni kufuata taratibu zilizopo kama kutoa notisi kwa chama alichotoka ili apate uthibitisho wa kuhama kwake na pia mwajiri ajulishwe.Muonekaano wa Jengo la Halmashauri ya Jiji la Dodoma,

.........................................................

Jambo hili ni kubwa na lina sura ya kitaifa kulingana na uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wetu, kuna Halmashauri nyingi ambazo walimu wamezuiwa kuondoka CWT na kujiunga CHAKAMWATA licha ya chama hicho kuwepo kisheria.


Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Vallence Wambali akizungumzia suala hilo alikiri kuwepo kwa Waraka huo 1/2022 unaodaiwa kutumiwa  na Wakurugenzi kuwazuia Walimu kujiunga na CHAKAMWATA.


Wambali alisema Waraka huo unatekelezwa na vyama vyote 35 vilivyo chini ya ofisi yake na kuwa kujiunga na chama chochote ni hiari ya mfanyakazi husika yeye hahusiki.


“Mwanachama anapojiunga nacho anapaswa kujisajili mwenyewe kwenye fomu maalumu,” alisema Wambali


Aidha, Wambali katika ufafanuzi wake  aliwataka viongozi wa vyama hivyo kufuata katiba na miongozo mbalimbali iliyowekwa pamoja na kuangalia maslahi ya wanachama, mwajiri na iwapo chama kitakuwa cha kitaifa kitoe huduma kwa wanachama wake wote.


“Mimi nikiwa mwangalizi wa vyama hivi nimekuwa nikifanya vikao vya mara kwa mara na viongozi wa vyama kwa ajili ya kukumbushana mambo mbalimbali ili kuvijenga, lengo likiwa kuviona vinakua,” alisema Wambali.


Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu kwa zaidi ya miezi mitatu sasa umebaini kuwa mpaka leo hii hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na wakurugenzi hao za kuwaruhusu walimu wanaotaka kuhamia CHAKAMWATA kutoka CWT na kuanza kuwaingizia michango ya 1% kwenye mishahara yao.


Aidha, uchunguzi huo ubebaini kuwa Waraka huo ambao Msajili wa vyama vya Wafanyakazi amekiri kuwa upo na unapaswa kufuatwa na vyama vyote, ndiyo unaolalamikiwa na Walimu kuwa unapingana na Sheria.


Waraka huo umedaiwa kutumiwa na Wakurugenzi kuwazuia Walimu kutumia uhuru wao wa kisheria wa kuchagua vyama vya walimu vya kujiunga navyo kama CHAKAMWATA na unatumika kuwalazimisha walimu kuwa wanachama wa CWT kwa lazima hata kama hawapendi.


Jambo hilo la kuwazuia walimu kutojiunga na chama wanachokitaka limedaiwa kuingiliwa na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kuwapinga kujiunga na CHAKAMWATA na chama wanachokitambua ni CWT.


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego Aprili 18, 2026 alipokuwa kwenye siku ya wadau wa Elimu mkoani humo iliyofanyika Shule ya Msingi Samamba Kijiji cha Utaho, Kata ya Kituntu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi anadaiwa kusema hadharani kuwa hakitambui CHAKAMWATA bali CWT hatua ambayo imelalamikiwa na walimu.


Hata hivyo, alipopigiwa simu mara kadhaa kwa nyakati tofauti ili kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (meseji) hakujibu.


Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma William Ndile ambaye anadaiwa na walimu hao kuwa alitoa maelekezo kwa wakurugenzi na maafisa Utumishi katika moja ya mikutano yake kuhakikisha zoezi la kuwasajili walimu hao kujiunga na CHAKAMWATA wanalifanya polepole licha ya kujua chama hicho kipo kisheria.


Alipopigiwa simu na mwandishi wetu ili kutoa ufafanuzi wa jambo hilo alisema hakumbuki chochote kuhusu jambo hilo na kuwa anafanya kazi kwa kufuata barua.


“Sisi viongozi tunafanya kazi kwa kufuata barua iliyosainiwa kama hao wanaolalamika wanayo wakuoneshe labda ningekuwa ofisini ningeweza kuangalia kwenye mafaili lakini sasa nipo likizo hivi ni kweli mkuu wa wilaya anaweza kuwazuia walimu wanaotaka kujiunga na chama wanachokitaka,” alihoji Ndile.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Adolf Ndunguru alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo, alimtaka mwandishi wetu ampigie Afisa Habari wa TAMISEMI kwa ufafanuzi.


Mwandishi wetu alipompigia simu afisa habari aliyefahamika kwa jina la Projestus Binamungu alisema anayepaswa kuzungumzia jambo hilo ni mkuu wa kitengo cha habari TAMISEMI na kuwa yeye ni afisa habari wa kawaida.


Hata hivyo, Binamungu alisema  jambo hilo lilipaswa kushughulikiwa na Katibu Mkuu ambaye ndiyo mwajiri wa walimu.


“Kwa kukusaidia tu, watu ambao wanaweza kulizungumzia suala hilo ni Tume ya Utumishi wa Walimu na ndiyo wanaotetea maslahi yao,” alisema Binamungu.


Aidha, alishangaa kuona jambo ambalo limefika kwa katibu mkuu  kurudishwa chini kwa ajili ya kulitolea majibu.Muonekano wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli mkoani Tanga.

...............................

Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya Simu 0754362990.
👇

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad