𝐁𝐀𝐑𝐑𝐈𝐂𝐊 𝐊𝐈𝐎𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐔𝐅𝐔𝐍𝐆𝐀𝐉𝐈 𝐌𝐈𝐆𝐎𝐃𝐈 𝐔𝐍𝐀𝐎𝐙𝐈𝐍𝐆𝐀𝐓𝐈𝐀 𝐕𝐈𝐖𝐀𝐍𝐆𝐎 𝐕𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐌𝐀𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐍𝐂𝐇𝐈𝐍𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, September 7, 2026

𝐁𝐀𝐑𝐑𝐈𝐂𝐊 𝐊𝐈𝐎𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐔𝐅𝐔𝐍𝐆𝐀𝐉𝐈 𝐌𝐈𝐆𝐎𝐃𝐈 𝐔𝐍𝐀𝐎𝐙𝐈𝐍𝐆𝐀𝐓𝐈𝐀 𝐕𝐈𝐖𝐀𝐍𝐆𝐎 𝐕𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐌𝐀𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐍𝐂𝐇𝐈𝐍𝐈

Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kutoka mkoani Njombe wamefanya ziara ya kikazi katika mgodi wa Barrick Buzwagi wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga uliopo katika mchakato wa kufungwa na kupongeza ufungwaji huo kufanyika kitaalamu kwa viwango vya kimataifa na kuacha urithi endelevu ikiwemo eneo la mgodi kugeuzwa kuwa kongani ya viwanda –Special Economic Zone.

Akiongea kuhusu na ziara hiyo, Mwenyekiti wa ALAT , Njombe , ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ALAT taifa, Agnetha Mpangile amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza utekelezaji na uendeshaji wa miradi kupitia sera na kanuni ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi kama ambavyo Barrick nchini imefanikisha kutekelezwa kwa miradi yenye tija katika maeneo yanayozunguka migodi yake yake.

"Tumekuja hapa Buzwagi japo mgodi tumekuta upo katika hatua ya mwisho kufungwa lakini tumeshuhudia ufungwaji wa mgodi ulivyofanyika kitaalamu na kuacha alama kubwa ya kiikolojia ya mazingira  na tunaipongeza Serikali  kwa kuligeuza eneo la mgodi kuwa Ukanda Maalum wa Kiuchumi (SEZ)", amesema.

Mpangile amesema  ujumbe huo wa ALAT  ujumbe huo umetembelea maeneo mbalimbali ambayo kwa sasa yana mandhari ya kuvutia na mazingira bora na endelevu ambayo yataendelea kuleta manufaa kwa jamii inayozunguka eneo hili na wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika kongani ya Buzwagi Special Economic Zone, ambayo tayari imeishaanza kuwa na mwekeleo kwa kuwa kitovu cha biashara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.


Vilevile umetembelea miradi ya CSR iliyotekelezwa na mgodi inayoendelea kuleta manufaa kwa wananchi.

“Moja ya funzo kubwa ni jinsi miradi hii ya kijamii ilivyotekelezwa kwa ufanisi mkubwa na usimamizi wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na ushirikishwaji wananchi kwenye kuibua miradi husika ni mfano wa kuigwa kwenye halmashauri , manispaa na majiji yetu,” amesema Mpangile.


Akitoa maelezo ya ufungaji mgodi kwa ujumbe huo kwa niaba ya Meneja Ufungaji wa  Mgodi wa Buzwagi, Afisa Mahusiano ya Jamii wa Barrick, Yunia Wangoya amefafanua kuwa, Barrick itaendelea kushirikiana na Serikali wakati wote kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa kwa kufunga shughuli za mgodi na kuacha eneo lililokuwa mgodi linakuwa na miradi endelevu ya kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.

“Jukumu la Kampuni endelevu ya uchimbaji madini si kutengeneza thamani kwa wadau wakati uliopo bali pia ni kuhakikisha kuwa inaacha urithi mzuri ambao utaendelea kuhudumia jamii kwa muda mrefu baada ya uchimbaji kufikia mwisho katika mgodi wa Barrick Buzwagi”,ameongeza Wangoya.

Vilevile ameueleza ujumbe huo kuwa mambo mengine ambao mgodi huo umetekeleza  ni miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa maji safi na salama wa chujio la maji ya mvua eneo la Mwendakulima uliopo chini ya Mamlaka ya Maji Kahama (KUWASA) utakaogharimu shilingi bilioni 4.8 ambao ukikamilika unatarajia kuhudumia zaidi ya asilimia 66 ya wakazi wa manispaa ya Kahama na kuondoa changamoto ya upungufu wa maji.

Barrick pia imeboresha uwanja wa ndege wa Kahama ambao kwa sasa una uwezo wa kuhudumia abiria kati ya 200 hadi 250 kwa wakati mmoja, hatua inayorahisisha usafiri wa anga na biashara.

Aidha Barrick Buzwagi imewezesha wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mgodi kuanzisha miradi ya kilimo endelevu ikiwemo miradi ya ufugaji nyuki na kuku kwa vijana na Wanawake.

Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi ulikuwa kitovu cha uchumi wa mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania kwa takribani miaka 15 ambapo katika kilele chake, Buzwagi ulikuwa mgodi wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania na uliajiri watu 3,000 na maisha yake ya uendeshaji yalifika tamati Julai 2021 na mgodi huo ulifungwa rasmi Julai 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad