ZAIDI YA MIL 700 ZA BIASHARA YA KABONI ZAJENGA KITUO CHA AFYA KATUMA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, October 19, 2026

ZAIDI YA MIL 700 ZA BIASHARA YA KABONI ZAJENGA KITUO CHA AFYA KATUMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akimkabidhi chandarua Mwananchi wa Kata ya Katuma Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi baada ya kukagua mradi wa Kituo cha afya kilichojengwa kutokana na fedha za Biashara ya Kaboni.
Baadhi ya majengo ya Kituo cha afya Kata ya Katuma Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kilichojengwa kutokana na fedha za Biashara ya Kaboni.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ni Mhe. Onesmo Buswelu akifafanua jambo wakati ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni kukagua mradi wa Kituo cha afya Kata ya Katuma kilichojengwa kutokana na fedha za Biashara ya Kaboni, Oktoba 18, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Mhe. Onesmo Buswelu mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya ziara ya kikazi, Oktoba 18, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza na Wananchi wa Kata ya Katuma Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi mara baada ya kukagua mradi wa Kituo cha afya kilichojengwa kutokana na fedha za Biashara ya Kaboni, Oktoba 18, 2026.

PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

*WILAYA YA TANGANYIKA YAVUNA MATUNDA YA BIASHARA YA KABONI, UJENZI WA KITUO CHA AFYA KATUMA WAKAMILIKA*

*NA; MWANDISHI WETU*

*KATAVI*

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo sita ya kutolea huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Katuma, kupitia fedha zinazotokana na Biashara ya Kaboni katika vijiji vya Katuma, Kapanga na Mpembe.


Mradi huo wenye zaidi ya thamani ya Shilingi milioni 700 ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Kata ya Katuma na maeneo jirani, huku ukidhihirisha manufaa ya uhifadhi wa mazingira kupitia biashara ya kaboni.


Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, katika Kata ya Katuma Oktoba 18, 2026, Katibu wa Kamati ya Ujenzi na Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Bw. Pascal Masobeji, amesema mradi huo umefanikiwa kukamilisha majengo muhimu yanayohitajika katika utoaji wa huduma za afya.


Amesema Kata ya Katuma ilipokea fedha hizo kwa awamu mbili. Katika awamu ya kwanza, iliyohusisha mgao wa awamu ya nne na ya sita, kata ilipokea Shilingi milioni 168 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD).


Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umeimarisha ushirikiano kati ya Kata ya Katuma na vijiji vinavyonufaika na Biashara ya Kaboni, huku ukionesha namna fedha zinazotokana na uhifadhi wa mazingira zinavyoweza kuelekezwa katika miradi ya kijamii yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.


Kwa upande mwingine, wananchi wa Kata ya Katuma wameeleza shukrani zao kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuwezesha jamii kunufaika na Biashara ya Kaboni.


Kukamilika kwa majengo hayo ni hatua muhimu katika maandalizi ya kuimarisha huduma za afya katika eneo hilo, huku kukiwa na matarajio ya kupunguza changamoto za wananchi kupata huduma za afya karibu na makazi yao.


Aidha, Waziri Masauni ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira na kukitumia vizuri Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ili kusajili miradi na kupata elimu juu ya Biashara hiyo.


“Serikali itaendelea kusimamia ili kuona jamii inanufaika na miradi hii kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika imekuwa mfano wa kuigwa katika Biashara ya Kaboni ambapo imefungua njia kwa wengine kufanya Biashara hii.” Amesema Waziri Masauni.


Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mgawanyo wa mapato yatokanayo na Biashara ya Kaboni ili jamii izidi kunufaika na kuendelea kulinda na kutunza mazingira

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad