Aprili 16, 2025 imekua ya baraka kubwa kwa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera baada ya kupata ugeni mzito wa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro aliyefanya shughuli ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Kata ya Katerero na Kemondo na baadae kufanya mkutano mkubwa wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Waziri Ndumbaro alianza ziara kwenye Tarafa ya Katerero kwa kukagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kisasa ya Amali ya Katerero iliyogharimu milioni 584 ikiwa na madarasa ya kutosha, maabara 3 za sayansi, maktaba, ICT room pamoja na ujenzi wa zahanati ya kijiji Mulahya iliyogharimu milioni 142,300,000 huku wakisubiliwa wahudumu tu na kumalizia choo na kichomea taka ili wananchi wa kijiji hichi ambao hawajawahi kuwa na huduma ya afya waanze kupata huduma kwenye kijiji chao.
Aidha, Waziri Ndumbaro alitembelea pia mradi mkubwa wa maji wa Kemondo- Maruku wa Bilioni 15.8 utakaonufaisha kata 7 huku wananchi wa kata baadhi wakiwa wameanza kupata huduma ya maji kupitia mradi huu mkubwa unaotumiwa Ziwa Victoria kama chanzo chake.
Jioni, Waziri alihitimisha ziara yake kwenye Tarafa ya Katerero kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara kwenye kata ya Kemondo pale sokoni Kemondo ambapo alizindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba huku akitumia mkutano huo kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Maeneo yote, wananchi walimpa salamu za shukrani za kumfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoleta miradi mikubwa ya maendeleo na Msaada wa Kisheria bure kwenye maeneo yao huku wakimuahidi kura zote kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2025 mwezi Oktoba.












No comments:
Post a Comment