LEO NI SIKU YA HUZUNI, FURAHA KWA WASHINDI WA KURA ZA MAONI CCM - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, August 20, 2025

LEO NI SIKU YA HUZUNI, FURAHA KWA WASHINDI WA KURA ZA MAONI CCM

Halmashauri kuu ya chama hicho kuteua jina moja

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Katibu wa chama hicho Taifa, Dkt. Emmanuel Nchimbi katika moja ya matukio ya chama hicho.

....................................... 

Na Dotto Mwaibale    

Leo macho na masikio ya watanzania na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanaelekezwa Jijini Dodoma ambapo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kitakachofanyika Ukumbi wa White House jijini humo.

Ajenda kuu ya kikao hicho ni kufanya Uteuzi wa Mwisho wa Wagombea nafasi za Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge Viti Maalum, Baraza la wawakilishi Zanzibar na Baraza la wawakilishi Viti Maalum.

Kikao cha kamati kuu cha chama hicho ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi  ambacho leo kinakwenda kupeleka furaha kwa watakao teuliwa na vilio kwa watakaoachwa wa nafasi ya ubunge katika kura za maoni.

Kikao hicho kitamteua mgombea mmoja kwa ajili ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge na wagombea wa vyama vingine katika uchaguzi mkuu.

Licha ya wagombea hao kupita kwa kura nyingi za wajumbe kwenye kura za maoni kikao hicho kitaangalia mambo mbalimbali ya wagombea hao.

Mambo hayo ni kama vile kukubalika kwa wananchi, iwapo mgombea husika kama alishinda kura hizo kwa njia ya rushwa na mambo mengine.

Lakini licha ya kikao hicho kuwa ndio cha mwisho kwa kutoa maamuzi kinapaswa pia kuangalia maamuzi ya wananchi waliowachagua wagombea wao wanaowataka tena kwa kura nyingi vinginevyo kuna hatari ya kutokea changamoto ya kuwakataa wale watakaoteuliwa na kikao hicho.

Kuna mifano ambayo tumeiona katika maaeneo mengi wakati wa uteuzi wa wagombea nafasi ya udiwani baada ya vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu za Wilaya na Mikoa kuwapitisha wagombea ambao wananchi hawakuwa chaguo lao.

Wananchi hao walikuwa wakiandamana kwenda ofisi za chama hicho na kupinga maamuzi ya vikao hivyo vya juu kwa kuwateulia wale ambao hawakuwa chaguo lao.

Tuliona jinsi vikao hivyo vilivyo lazimika kuketi tena na kuwarejesha wagombea waliokuwa wakitakiwa na wananchi.

Jambo hilo lilipaswa kuangaliwa kwa umakini kabla ya kuwateua wagombea hao ambao hawakubaliki na wananchi hatua ambayo itasaidia kupunguza malalamiko kwa wagombea na wananchi kwa ujumla na muda.

Athari za kuwapekea wananchi viongozi ambao hawawataki ni kubwa mno kwani wanaweza kukisusia chama na hata kutompa ushirikiano mbunge ambaye hawakumtaka jambo ambalo litafifisha maendeleo kwenye jimbo husika na Taifa kwa ujumla.

Tuna imani na kikao hicho kutokana na kuwa na timu makini chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Samia hivyo tunatoa rai kwa wagombea kuyaheshimu maamuzi yatakayofikiwa.

Wagombea wanaaswa kuzingatia utaifa na uzalendo kwani katika uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa na kuna mambo ya muhimu yanaangaliwa kabla ya kuteuliwa na hakuna upendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad