MFUKO WA SELF KUTOA MIKOPO YA BILIONI 300 HADI KUFIKIA 2030 August 15, 2025 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, August 15, 2025

MFUKO WA SELF KUTOA MIKOPO YA BILIONI 300 HADI KUFIKIA 2030 August 15, 2025


 
Na Salum Mnette

KATIKA kutimiza majukumu yake kwa ufanisi Mfuko wa SELF (Self MF) umekusudia kutoa mikopo ya shilingi bilioni 300 ndani ya miaka mitano na kuwafikia wanufaika 200, 000 nchini kote. 

Hayo yamesemwa leo, Agosti 15, 2025 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Bi. Santiel Yona, katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari, uliofanyika katika Hoteli ya KingJada na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina.

‘’Ili kutimiza majukumu yetu kwa ufanisi mfuko umejiwekea malengo  makuu matatu katika mpango mkakati wake, ikiwemo kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wa kipato cha chini na kutoa elimu ya fedha,’’ alisema Bi. Santiel.

Alisema, katika kipindi cha miaka mitano (2026 hadi 2030) mfuko unapanga kutoa mikopo ya shilingi bilioni 300 na kuwafikia wanufaika 200,000 nchini.

Pamoja na kutoa mikopo hiyo, Mtendaji Mkuu huyo alisema, mfuko huo unakusudia kuongeza matawi  kutoka 12 hadi 22 kufikia 2030.

‘’Hii ni kuongeza ufanisi  (operational efficiency) ili kutoa huduma bora na kwa wakati. Hii litawezekana kwa kubadilisha mifumo na kutumia zaidi teknolojia,’’ alisema.

Alisema, lengo lingine walilojiwekea ni uendelevu wa taasisi kimapato (financial sustainability ) ambapo watasimamia utoaji wa huduma bora ili kuhakikisha mikopo inarejeshwa, taasisi inajiendesha kwa faida na huduma zinazotolewa zinakuwa  endelevu.

Akifafanua zaidi majukumu ya mfuko huo, alisema ni kutoa huduma za mikopo midogo kwa watu  binafsi, vikundi na taasisi ndogo za fedha zinazolengwa na serikali ili kulea na/au kukuza sekta ya ndogo za kifedha kwa ajili ya kupunguza umaskini.

Majukumu mengine ni kutambua, kuendeleza na kukuza fursa za kuwezesha ajira kwa wajasiriamali wadogo na taasisi za huduma ndogo za fedha, elimu ya utendaji kazi na mafunzo kwa ajili ya kuboresha stadi zao.

Kuandaa na kuweka utaratibu  na mikakati ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa ajili ya kujiajiri kwa tija.

Akielezea kuhusu huduma zao, Bi. Santiel alisema mfuko huo unatoa mikopo kwa njia mbili, mikopo kupitia taasisi ndogo za fedha (wholesale lending) ili kusaidia kutoa mikopo kwa wateja walengwa wa SELF na mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika (direct lending).

Kutoa elimu ya fedha na kujengea uwezo taasisi za huduma ndogo za fedha, ambapo mteja mmoja mmoja hupatiwa elimu ya fedha na taasisi za huduma ndogo za fedha, pia hupewa mafunzo ya kujengewa uwezo wa kuendesha taasisi zao.

Akizungumza kuhusu huduma ya uwakala wa bima, alisema wanahamasisha wananchi kujikinga na  majanga kwa kukata bima. ‘’Kuna bima ya mikopo na bima za kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali  kama vile moto, wizi na kadhalika,’’ alisema.

Alisema, Mfuko wa SELF  unatoa mikopo ya aina nyingi ikiwemo mikopo kwa taasi za huduma ndogo za fedha MF Ls/SACCOS. 

‘’Mikopo hii inalenga wanufaika wanaofanya biashara au kilimo. Ipo pia mikopo ya moja kwa moja kwa  wanufaika, ambapo walengwa wa mikopo hii ni wajasiriamali wadogo na wakati, wakulima wadogo, wafugaji kwa ajili ya kuboresha makazi kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na mikopo kwa ajili ya watumishi wa umma,’’ alisema.

Akielezea kuhusu mafanikio waliyoyapata kama mfuko, alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021  hadi Juni 30,  2025, mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 196.9 na kwa kiwango cha mikopo chechefu  kikiwa chini ya asilimia 10 na pia mfuko kuweza kujiendesha kwa kupata faida.

‘’Mikopo imewafikia wanufaika  wapatao 183,381, kati yao wanawake ni  97,170, sawa na asilimia 53 na wanaume ni 86,211, sawa na asilimia  47,’’ alisema.

Aliongeza, toka mwaka 2021 mpaka Juni 30, 2025 mfuko umezikopesha na kuzijengea uwezo taasisi 549 za huduma ndogo za fedha. 

Hata hivyo, alisema kuzijengea uwezo wa taasisi hizi katika masuala ya huduma ndogo za fedha kunasaidia kupunguza changamoto za uendeshaji wake.

Alisema, mfuko umesaidia kutengeneza ajira kwa wakopaji wao wenyewe na wale wanaowaajiri, kiasi cha ajira 183,381 kimetengenezwa kutoka mwaka 2021 hadi Juni 2025.

Mtendaji Mkuu huyo alisema, katika kutekeleza majukumu yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wa kipato cha chini, mfuko huo unakumbana na changamoto kadhaa.

Changamoto hizo ni pamoja na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya fedha ambayo husababisha kukosa uelewa wa kutosha  wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa mikopo au kutumia mikopo nje ya malengo yaliyokusudiwa.

‘’Wananchi wengi kutokuwa na utamaduni wa kukopa na kurejesha, kwani utamaduni wa kurejesha mikopo kwa hiyari bado ni mdogo,’’ alisema.  

Changamoto nyingine ni wananchi wengi wa kipato cha chini hujishughulisha na biashara zisizo rasmi, hii inatoa changamoto katika kuwakopesha.   

SELF MF ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo kwa wananchi hasa wa kipato cha chini wanaojishughulisha  na shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza umasikini

Mfuko huu ulianza kutekeleza majukumu yake Julai Mosi, 2015 ukirithi majukumu ya mradi wa serikali uliojulikana kama SMALL ENTREPRENEURS LOAN FACILITY (SELF) PROJECT. Mradi ulitekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia  mwaka 2000 hadi 2015.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad