Na Dotto Mwaibale, Singida
SHEIKH wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro amesema Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Singida imeweka hisoria kubwa
kwa kuandaa Iftar kwa wadau wake mkoani humo.
Kiongozi huyo mkuu wa dini ya kiislamu mkoani Singida Sheikh
Nasoro aliyasema hayo wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa
wa Singida iliyofanyika leo Machi 18, 2026 na kuandaliwa na wadau wa taasisi
hiyo mkoani hapa.
“TAKUKURU Singida jambo la kufuturisha mlilolifanya halijawahi kufanyika mkoani hapa hakika mmeweka historia kubwa,” alisema Sheikh Nasoro.
Aidha, Sheikh Nasoro alisema jukumu la kuzuia na kupambana
na rushwa ni la lako na langu hivyo kila
mmoja kwa nafasi yake atimize jukumu hilo.
Akizungumzia suala la rushwa Sheik Nasoro alisema hata Mtume
Muhammad (SAW) alilikemea na kufika mbali zaidi kwa kueleza alaaniwe mtu
aliyetoa na kupokea rushwa na anayefanya hivyo ajitambue yupo katika laana ya
Mwenyezi Mungu.
Alisema katika taifa kuwa na watu wenye laana ni angamizo
kubwa kwenye jamii hivyo ni vizuri kuikwepa laana hiyo kwa kuacha kufanya
vitendo vya rushwa.
Sheikh Nasoro aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wa kiislam
ambao wamepewa kutoa maamuzi wamekuwa wakifanya vitendo vya rushwa kwa kupokea
rushwa na kupindisha haki jambo ambalo siyo zuri mbele ya Mwenyezi Mungu.
Alisema jambo hilo limekuwa likifanyika kwa watoa maamuzi
wanaotatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ndoa ambapo wanawake na wanaume
wamedaiwa kutoa rushwa ili washinde na kuwaacha wenza wao ili wabaki huru.
“Baada ya kupata ushindi kwa kutoa rushwa baada ya siku kadhaa utakuta ameolewa na yule mtoa maamuzi aliyempa rushwa na kushinda kesi dhidi ya mumewe na vilevile kwa mwanaume kwenda kuoa wakati shauri hilo lingeweza kusuruhishwa kwa haki na maisha yao yakaendelea bila ya kuwa na athari,” alisema Sheikh Nasoro na kuiomba TAKUKURU kulichunguza.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Petro Horombe akizungumza
wakati wa Iftar hiyo iliyoandaliwa na taasisi hiyo alisema imelenga kuwahusisha
wadau wao wa Mkoa wa Singida.
“Sisi Watumishi wa TAKUKURU ni sehemu ya jamii na ndiyo
maana mmekuwa mkituona tukifanyakazi na jamii ikiwa ni pamoja na kutoa misaada
mbalimbali ya kijamii na Iftar hii ni sehemu ya matendo tunayofanya,” alisema
Horombe.
Mgeni rasmi wa Iftar hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson
alisema katika utumishi wake wa miaka saba kwa nafasi ya ukuu wa wilaya na miaka
mitano ya ubunge hajawahi kuona upendo wa namna hiyo.
“Sijawahi kuona upendo wa aina hii waliotufanyia hawa ndugu zetu wa TAKUKURU kwani wangeweza kujifanyia wenyewe lakini wakaona vizuri watushirikishe tunashukuru sana,” alisema Apson.
Apson alisema suala la mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
la muhimu sana na kuwa linatukumbusha uwepo wa Mwenyezi Mungu na majukumu ya
Uislaam kama amani, kusamehana, kufanya dua na kufuata maandiko yaliyopo kwenye
Quran,” alisema Apson.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Petro Horombe akizungumza wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa wadau wake.




















No comments:
Post a Comment