𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐋𝐀𝐏𝐈𝐓𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐁𝐀𝐉𝐄𝐓𝐈 𝐘𝐀 𝐖𝐈𝐙𝐀𝐑𝐀 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐘𝐀 𝐍𝐉𝐄 𝐍𝐀 𝐔𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈𝐀𝐍𝐎 𝐖𝐀 𝐀𝐅𝐑𝐈𝐊𝐀 𝐌𝐀𝐒𝐇𝐀𝐑𝐈𝐊𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, May 28, 2026

𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐋𝐀𝐏𝐈𝐓𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐁𝐀𝐉𝐄𝐓𝐈 𝐘𝐀 𝐖𝐈𝐙𝐀𝐑𝐀 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐘𝐀 𝐍𝐉𝐄 𝐍𝐀 𝐔𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈𝐀𝐍𝐎 𝐖𝐀 𝐀𝐅𝐑𝐈𝐊𝐀 𝐌𝐀𝐒𝐇𝐀𝐑𝐈𝐊𝐈

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2026/2027 baada ya kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, aliliomba Bunge kupitisha jumla ya shilingi 359,326,404,000 ili kutekeleza majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kombo alieleza kuwa kati ya fedha hizo, shilingi 312,961,378,000 zitatumika kwa Matumizi ya Kawaida, wakati shilingi 46,365,026,000 zimetengwa kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

Baada ya mjadala wa wabunge, Bunge limepitisha rasmi makadirio hayo ya bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Waziri Kombo alilieleza Bunge kuwa Tanzania imeendelea kudumisha misingi ya uhusiano na ushirikiano wa kimataifa, kama ilivyowekwa na waasisi wa Taifa na kuainishwa katika Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la 2024.

Alitaja Misingi hiyo kuwa ni Kulinda Mamlaka kamili ya nchi, mipaka kamili na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Kulinda uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia; Kukuza ujirani mwema; Kukuza Umoja wa Afrika; Kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo; Kuwezesha utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote na Ushirikiano wa nchi zinazoendelea; Kuunga Mkono Umoja wa Mataifa katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama; na Kulinda maadili, mila, desturi na utamaduni wa watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Misingi hii imechangia kudumisha heshima na taswira njema ya Taifa letu kupitia ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa,” alisisitiza Balozi Kombo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad