𝐔𝐖𝐄𝐊𝐄𝐙𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐈𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐘𝐀 𝐓𝐄𝐇𝐀𝐌𝐀 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈𝐍𝐈 𝐊𝐔𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐍𝐈𝐒𝐈 𝐍𝐀 𝐔𝐖𝐀𝐙𝐈 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐔𝐓𝐎𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐇𝐔𝐃𝐔𝐌𝐀 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, May 19, 2026

𝐔𝐖𝐄𝐊𝐄𝐙𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐈𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐘𝐀 𝐓𝐄𝐇𝐀𝐌𝐀 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈𝐍𝐈 𝐊𝐔𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐍𝐈𝐒𝐈 𝐍𝐀 𝐔𝐖𝐀𝐙𝐈 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐔𝐓𝐎𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐇𝐔𝐃𝐔𝐌𝐀

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akizungumza na viongozi, na Watumishi wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (eGovRIDC), mara baada ya kuwasili na kutembelea miradi mbalimbali ya kituo hicho Mei 18, 2026 jijini Dodoma
Menejimenti na Watumishi wa Taasisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba (hayupo pichani) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray kuhusu utendaji wa kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (eGovRIDC) kilichopo Jijini Dodoma.
-----------------------------

Tarehe 18/05/2026

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesema uwekezaji wa matumizi ya Mifumo ya Tehama Serikalini utasaidia kwa asilimia kubwa kuongeza ufanisi na Uwazi wa huduma zinazotolewa na Watumishi wa umma kwa wananchi kwa maslahi ya Taifa

Mhe. Qwaray ameyasema hayo Mei 18, 2026 wakati akizungumza na Uongozi wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (eGovRIDC), Menejimenti pamoja na Watumishi kutoka Taasisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) mara baada ya Naibu Waziri huyo kutembelea Kituo hicho Jijini Dodoma.

“Ni lazima tufahamu kwamba, katika dunia ya sasa, mageuzi ya kidijiti si chaguo tena bali ni msingi wa ufanisi wa Serikali, ushindani wa kiuchumi na maendeleo ya kijamii”. Mhe. Qwaray alisema.

Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, kupunguza urasimu na rushwa, kuongeza uwazi, na kurahisisha upatikanaji wa huduma za wananchi popote walipo.

Mhe.Qwaray ameongeza kuwa, Serikali imepata mafanikio makubwa katika matumizi ya mifumo ya Kidijiti katika Sekta mbalimbali ikiwemo kuongeza uwajibikaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha utendaji kazi wa Utumishi wa Umma.

Aidha, Mhe Qwaray amesema kituo hicho kimekuwa na mchango chanya katika matumizi ya Mifumo mbalimbali kama vile Mfumo wa wa kielektroniki unaoiwezesha Serikali kupokea na kushughulikia malalamiko, maoni, pongezi, na maulizo kutoka kwa wananchi kwenda kwenye taasisi zote za umma (e-Mrejesho) pamoja na Mfumo wa Dirisha la Huduma za Serikali ikiwemo tangazo la Gazeti la Serikali na Utoaji wa Vibali vya Likizo bila Malipo.

Mhe. Qwaray ametoa wito kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)

kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Vyuo Vikuu, taasisi za tafiti pamoja na Sekta Binafsi ili tafiti zinazofanyika ziweze kutatua changamoto halisi za wananchi na taasisi za umma.

Vilevile ameitaka Taasisi hiyo kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni, na Miongozo ya Serikali Mtandao ili mifumo yote inayotengenezwa iwe salama, yenye kuwasiliana na mifumo mingine na kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ilianzisha Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (e-GOVRIDC) kwa lengo la kuratibu shughuli za kitafiti, kubuni na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao, ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa umma, kuwajengea uwezo na kukuza vipaji vya vijana wabunifu katika eneo la TEHAMA. 

Mhandisi Ndomba amemshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray kwa kuitikia wito wa kutembelea kituo hicho na kuahidi kwamba wameyapokea na wataenda kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kiongozi huyo. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad