Na Mwandishi Wetu.
WAKAZI wa Kitongoji katika Kijiji cha Homboza, Kata ya Msimbu, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, wamedai kutishiwa amani baada ya nyumba zao kuwekewa alama ya X na viongozi wao na kutakiwa kuondoka.
Wakizungumza leo Jumapili, mmoja wa wakazi hao, Halima Said alidai kwamba ameshangazwa na viongozi wa serikali ya kijiji, akiwamo mwenyekiti wao wa kitongoji, Omary Simba kufika katika makazi yao na kuweka alama X huku wakitakiwa kuondoka kwa madai eneo wanaloishi lina mgogoro.
Halima alidai kwamba Simba ambaye aliambatana na mtendaji wa kijiji hicho, Maida Lugoya, ameshangazwa na kauli ya viongozi hao, kwani inatishia amani, kwa sababu eneo analoishi alinunua kihalali.
Alidai kwamba viongozi hao wa kijiji walifika katika makazi yao kwa maelekezo ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, inayoongozwa na Petro Magoti.
Pia, alidai anashangaa kuona serikali ya kijiji inakuja na kauli hiyo wakati ndiyo iliidhinisha mauzo aliponunua kiwanja kutoka kwa mmiliki wa eneo hilo, Juma Kizeru.
Kwa upande wake, Fazil Seleman alidai Ijumaa wiki iliyopita walifika viongozi hao wa kijiji na kuambiwa wanaishi eneo la uvamizi.
Seleman alidai kama wanataka kujua halali wa eneo hilo waende kwa mkuu wa wilaya ambaye atakuwa Homboza, kwa kuwa ndiye aliyetoa oda ya kuweka X nyumba zao.
Balozi wa nyumba 10 wa Serikali ya Kijiji cha Homboza, Zainab Luneka na Katibu wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT), alidai katika mgogoro huo hakushirikishwa kwa lolote, licha ya kushuhudia viongozi wa juu wa kijiji hicho kufika katika eneo hilo na kuweka alama ya X kwa madai kwamba wamepewa maelekezo na uongozi wa juu wa wilaya.
Zainab alisema akiwa kiongozi wa eneo hilo, hajui mmiliki halali ni nani, ambalo linawakazi 18 waliojenga nyumba zao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Homboza, Omar Simba alikiri kutekeleza maagizo waliyopewa na uongozi wa Wilaya ya Kisarawe kuhusu sakata hilo.
Lakini mwenyekiti huyo, alikanusha madai ya wakazi hao kwamba wametakiwa kuondoka katika eneo hilo.
Simba alisema wakazi waliowekewa alama ya X katika nyumba zao, wanatakiwa kufika ofisini kwake ili kujua walipataje eneo hilo, baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa mtu mwingine.
"Sisi hatukuwaambia waondoke eneo hili, ila tunahitaji wafike ofisini," alisema Simba.
Mtendaji wa kijiji hicho, Maida alipotafutwa kwa njia ya simu hakutaka kuzungumzia lolote zaidi ya kumtaka mwandishi wa habari hizi kufika ofisini kwake kesho Jumatatu wiki hii, saa moja na nusu asubuhi kwa ufafanuzi zaidi. 










No comments:
Post a Comment