𝐊𝐔𝐄𝐋𝐄𝐊𝐄𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐇𝐈𝐌𝐈𝐒𝐇𝐎 𝐘𝐀 𝐌𝐈𝐀𝐊𝐀 𝟑𝟎,𝐓𝐑𝐀 𝐘𝐀𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀 𝐊𝐎𝐍𝐆𝐀𝐌𝐀𝐍𝐎 𝐋𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐈𝐋𝐈 𝐍𝐀 𝐕𝐈𝐎𝐍𝐆𝐎𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐃𝐈𝐍𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, June 18, 2026

𝐊𝐔𝐄𝐋𝐄𝐊𝐄𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐇𝐈𝐌𝐈𝐒𝐇𝐎 𝐘𝐀 𝐌𝐈𝐀𝐊𝐀 𝟑𝟎,𝐓𝐑𝐀 𝐘𝐀𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀 𝐊𝐎𝐍𝐆𝐀𝐌𝐀𝐍𝐎 𝐋𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐈𝐋𝐈 𝐍𝐀 𝐕𝐈𝐎𝐍𝐆𝐎𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐃𝐈𝐍𝐈

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupitia Idara ya Mambo ya Ndani (INAD), leo Juni 17, 2026 imeandaa Kongamano la Maadili lililowakutanisha viongozi wa dini mbalimbali kujadili nafasi ya maadili katika kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kujenga utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari. Kongamano hilo ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 30 ya TRA yatakayofanyika Julai 1, 2026.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Mcha Hassan Mcha, amesema kuwa katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TRA, taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, huku maadili yakiendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Bw. Mcha amesema TRA inaendelea kuwekeza katika mifumo na mikakati mbalimbali ya kuimarisha maadili kwa watumishi wake na walipakodi ili kujenga uaminifu, uwajibikaji na kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari.

“Maadili hujenga imani, na imani hujenga ulipaji wa kodi kwa hiari,” alisema Bw. Mcha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, ameipongeza TRA kwa kuandaa kongamano hilo na kueleza kuwa maadili ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na taifa. Amesema mafundisho ya dini yanasisitiza uadilifu, uwajibikaji na kufanya mema, huku ulipaji wa kodi ukiwa sehemu ya wajibu unaochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya nchi.

Naye Mkuu wa Evangelical Fellowship Church Tanzania, Askofu Charles Asher Howard, amesema maandiko matakatifu yanaelekeza waumini kutimiza wajibu wao kwa mamlaka halali, ikiwemo kulipa kodi. Amebainisha kuwa maendeleo ya Tanzania yanategemea mchango wa kila mwananchi, hivyo ulipaji wa kodi ni jukumu la pamoja linalopaswa kutekelezwa kwa uaminifu na uzalendo.

Viongozi hao wa dini wamepongeza hatua ya TRA ya kuwashirikisha katika mijadala ya maadili na ukusanyaji wa mapato, wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za umma na viongozi wa dini una nafasi muhimu katika kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari na kujenga taifa lenye uwajibikaji, uadilifu na maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad