MAISHA YA MATESO: MTOTO MWENYE USONJI AVUNJIKA MGUU, FAMILIA YALIA KUOMBA MSAADA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, June 19, 2026

MAISHA YA MATESO: MTOTO MWENYE USONJI AVUNJIKA MGUU, FAMILIA YALIA KUOMBA MSAADA

Dada wa Swaum Leila Shabani Mchora, akiwa amempakata mdogo wake nyumbani kwao baada ya kuvunjika mguu.

......................................

MAISHA ya mtoto Swaum Shabani Mchora (14), mkazi wa Mtaa wa Kibong'wa, Pugu Kwa Mustafa, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, yameendelea kuwa ya majonzi baada ya kukumbwa na tatizo jingine la kiafya la kuvunjika mguu, huku tayari akiwa anaishi na ugonjwa wa usonji tangu kuzaliwa.

Mama wa mtoto huyo, Sauda Selemani, amesema tukio hilo lilitokea alipokuwa ametoka kutafuta riziki za familia na kumwacha mtoto huyo akiwa nyumbani chini ya uangalizi wa dada yake.

"Usiku alianza kulalamika huku akishika mguu. Siku iliyofuata mguu ulianza kuvimba. Nilipompeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili walimpiga X-Ray na kugundua kuwa umevunjika. Naamini alianguka akiwa amelala," alisema Sauda.

Alisema hali ya mwanawe imeendelea kuwa mbaya kutokana na kushindwa kupata matibabu ya uhakika kwa sababu bima ya afya aliyonayo haiwezi kugharamia baadhi ya dawa na huduma muhimu zinazohitajika.

"Uwezo wa kununua dawa hizo sina. Mwanangu anazidi kudhoofu kila siku tofauti na mwanzo. Sijui nifanye nini zaidi ya kuona giza mbele yangu," alisema kwa huzuni.

Mbali na changamoto ya mtoto wake, Sauda amesema mumewe pia anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu unaomsababisha kuanguka mara kwa mara. Naye mwenyewe anasumbuliwa na maumivu ya goti la mguu wa kulia pamoja na matatizo ya pingili za mgongo yanayohitaji upasuaji.

"Hata kupata chakula cha familia ni changamoto. Sijui hatima ya maisha yetu itakuwaje," alisema.

Sauda amesema baada ya kuandika ombi lake la kuomba msaada kwenye mitandao ya kijamii Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi alipoona taarifa hiyo aliwatuma  maafisa ustawi wa jamii kutoka Hospitali ya Pugu ambao walifika nyumbani kwake na kuchukua maelezo ya changamoto anazopitia.

Hata hivyo, amesema hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

"Nikiwapigia simu wananiambia bado wanasubiri majibu kutoka juu," alisema.

Kwa mujibu wa Sauda, hali ya Swaum imezidi kuwa mbaya tangu alipoanguka..

Alisema madaktari walibaini kuwa mgongo wa mtoto huyo umepinda na kusababisha mbavu kubana, hali inayochangia ugumu wa kupumua.

"Daktari aliniambia ninunue vifaa viwili maalumu vya kumsaidia kunyosha mgongo ili mbavu ziachane na upumuaji wake urudi katika hali ya kawaida," alisema.

Alifafanua kuwa gharama za vifaa hivyo ni takribani Shilingi 850,000, fedha ambazo hana uwezo wa kuzipata.

Aidha, alisema licha ya kuwa na bima ya afya, mara nyingi hulazimika kununua dawa kwa fedha zake mwenyewe au kurejea nyumbani bila matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.

"Mara nyingi nakosa hata nauli ya kwenda na kurudi hospitali. Wakati mwingine naomba msaada kwa wauguzi, madaktari na wasamaria wema ili nifike nyumbani," alisema.

Mama huyo mwenye watoto watano amesema angepata mtaji wa biashara au msaada wa bima ya afya yenye kiwango kikubwa zaidi, hali ya familia yake ingeweza kubadilika.

"Daktari amesema mwanangu anaweza kuimarika akipata lishe bora, dawa na mazoezi ya mara kwa mara.

 Changamoto ni namna ya kupata fedha za kugharamia mahitaji hayo," alisema.

Changamoto nyingine ni usafiri wa dharura kwenda Hospitali ya Muhimbili nyakati za usiku pale mtoto anapozidiwa.

"Tunatoka Pugu Kwa Mustafa hadi Muhimbili usiku wa manane. Hilo nalo ni tatizo kubwa," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Shina Namba 2, Emanuel Zakaria, amethibitisha kuwepo kwa changamoto zinazoikabili familia hiyo.

"Tunafahamu hali ya Sauda na familia yake. Ni kweli wanahitaji msaada wa haraka kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na wasamaria wema," alisema.

Naye dada wa Swaum, Leila Mcharo, ambaye amemaliza kidato cha nne lakini ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa ada, ameomba nafasi yoyote ya kazi ili aweze kusaidia familia.

"Niko nyumbani. Nikipata hata kazi ya kuuza mafuta kwenye sheli nitafanya ili kusaidia familia na kuweka akiba ili nianze masomo ya Hotel Management," alisema.

Mtaalamu wa lishe, Mariam Ismail, amesema historia ya afya ya Swaum inaonesha dalili za changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa lishe bora, hali iliyochangia kudhoofika kwa mifupa na misuli yake.

Alisema mtoto huyo anahitaji mpango maalumu wa lishe wenye virutubisho muhimu kama Calcium, Vitamin D, Magnesium, Zinc na Omega 3, pamoja na ufuatiliaji wa karibu ili kusaidia kuimarisha afya yake.

Kutokana na hali hiyo, familia ya Sauda inaendelea kuomba msaada kutoka kwa Watanzania wenye uwezo ili kusaidia matibabu ya mtoto huyo pamoja na mahitaji mengine muhimu ya maisha.

Watakaoguswa kutoa msaada kwa mtoto huyo wanaweza kuwasiliana moja kwa moja na na Mama wa mtoto huyo Sauda Selemani Magwelo kupitia namba 0623757336 au 0625414791.

Msaada wowote, iwe fedha, chakula, sabuni, sukari au mahitaji mengine ya msingi, unaweza kuwa mwanga wa matumaini kwa familia hiyo inayopitia kipindi kigumu cha maisha.

Mama ya Swaum, Sauda Selemani akiwa amempakata mwanaye.
Mtoto Swaum akiwa amelala nyumbani kwao baada ya kuvunjika mguu.

......................................

Habari hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad