Na Godwin Myovela, Iringa
Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mwaka 2026 yamehitimishwa rasmi mkoani Iringa, yakiacha alama kubwa ya ushindani, nidhamu, umoja na matumaini mapya kwa kizazi cha vijana wenye vipaji.
Mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku 11 kuanzia Juni 06 hadi Juni 17, 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lugalo, yaliwakutanisha wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokuja kuonyesha uwezo wao katika michezo tofauti.
Zaidi ya ushindani wa medali na ushindi, UMITASHUMTA imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kubaini hazina ya vipaji vilivyofichika ndani ya watoto wa Kitanzania ambao wanaweza kuwa mabingwa wa kesho.
Akifunga mashindano hayo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha vipaji vinavyogunduliwa kupitia mashindano ya shule havipotei bali vinapata malezi na mazingira bora ya kukua.
Amesema michezo ya shule ni msingi wa kujenga wanamichezo bora, kwani ndipo safari ya mabingwa wengi wa kitaifa na kimataifa huanzia.
Kauli hiyo inaonesha mabadiliko ya mtazamo ambapo michezo haiangaliwi tena kama burudani pekee, bali ni sekta yenye uwezo wa kutengeneza ajira, kujenga afya, kukuza nidhamu na kuongeza heshima ya Taifa katika jukwaa la dunia.
Katika hatua ya kuimarisha mfumo huo, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuboresha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kukamilisha Akademia ya Taifa ya Michezo.
Uwekezaji huo unalenga kuunda kituo maalumu kitakachopokea vipaji vinavyobainika katika UMITASHUMTA na UMISSETA, kuvilea kitaalamu na kuviandaa kwa ushindani mkubwa zaidi.
Ni hatua inayotoa ujumbe kuwa mustakabali wa michezo Tanzania haupaswi kujengwa kwa bahati, bali kwa mipango, uwekezaji na mfumo endelevu wa malezi kuanzia ngazi za chini.
Mafanikio ya timu za vijana kama Serengeti Boys yameonesha kuwa uwekezaji katika mashindano ya shule unaweza kuzaa matunda makubwa pale vipaji vinapopewa nafasi, mwongozo na maandalizi sahihi.
Hata hivyo, safari ya mafanikio inahitaji zaidi ya kujenga miundombinu. Inahitaji uwekezaji katika makocha wenye ubora, vifaa vya kisasa, lishe bora kwa wanamichezo vijana, elimu ya afya na programu endelevu za maendeleo ya vipaji.
Mikoa na halmashauri nazo zinapaswa kuendelea kuimarisha michezo mashuleni kwa kuwa kila mtoto mwenye kipaji anahitaji nafasi ya kuonekana, kuaminiwa na kupewa mazingira ya kufikia ndoto yake.
UMITASHUMTA inapaswa kuendelea kuwa daraja la kitaifa la kuibua kizazi kipya cha wanamichezo watakaobeba bendera ya Tanzania katika mashindano ya Afrika Mashariki, Afrika na dunia.
Kwa upande mwingine, washindi na washiriki wanapaswa kuona mafanikio haya kama mwanzo wa safari mpya inayohitaji nidhamu, kujituma na kuzingatia elimu pamoja na michezo.
Hatma ya michezo Tanzania ipo katika namna Taifa litakavyowekeza leo kwa vijana wake. Kila uwanja wa shule, kila mashindano na kila kipaji kinachogunduliwa ni uwekezaji wa kesho wenye uwezo wa kuleta heshima, ajira na maendeleo kwa Taifa.
Kwa mafanikio ya UMITASHUMTA 2026 mkoani Iringa, ujumbe mkubwa umebaki wazi: Tanzania ina vipaji vingi; kinachohitajika sasa ni mfumo imara wa kuvitambua, kuvilinda na kuvigeuza kuwa nguvu ya maendeleo ya taifa.
















No comments:
Post a Comment