Na Godwin Myovela, Iringa
WAKATI Tanzania ikipiga hatua kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sauti mpya imeibuka kutoka kwa wadau wa elimu binafsi wakisisitiza kuwa mafanikio ya taifa hayawezi kupatikana ikiwa baadhi ya washirika muhimu katika sekta ya elimu wataendelea kukumbana na vikwazo vinavyodhoofisha mchango wao.
Hayo yalibainishwa katika mkutano wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), ambapo Kaimu Mwenyekiti wa TAMONGSCO Kanda ya Nyasa, Dk. Yahaya Msigwa, aliweka wazi changamoto zinazowakabili wawekezaji wa elimu huku akitaka mazingira yenye haki, usawa na utambuzi wa mchango wa sekta binafsi.
Dk. Msigwa alisema bado kuna baadhi ya halmashauri zinazoendelea kutoza kodi ambazo tayari zilifutwa na serikali, jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji wa shule na kupunguza ari ya uwekezaji katika sekta inayobeba sehemu kubwa ya matumaini ya kizazi kijacho.
Alionya kuwa endapo changamoto hizo hazitapatiwa ufumbuzi kwa wakati, zinaweza kuathiri juhudi za kuongeza ubora wa elimu, kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kupanua fursa za elimu kwa watoto wengi zaidi nchini.
Mbali na suala la kodi, Dk. Msigwa alieleza kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu wanafunzi wanaotoka shule binafsi kushindwa kupata nafasi stahiki katika shule za vipaji licha ya kufanya vizuri kwenye mitihani na kuonyesha uwezo mkubwa kitaaluma.
Kwa mujibu wake, hali hiyo imekuwa ikijenga hisia za kutotendewa haki kwa baadhi ya wanafunzi na wazazi wao, huku ikiibua maswali kuhusu usawa wa fursa katika mfumo wa elimu unaopaswa kuwapa nafasi sawa watoto wote bila kujali wanapotoka.
Alisema kinachoumiza zaidi ni kuwepo kwa lugha na mitazamo ya kibaguzi dhidi ya watoto wanaosoma shule binafsi, jambo ambalo huathiri kisaikolojia wanafunzi na kupunguza kujiamini kwa baadhi yao katika safari ya kutafuta mafanikio.
“Sisi si maadui wa serikali. Sisi ni wadau na washirika wa serikali katika malezi na elimu ya watoto wa Tanzania. Tunachokiomba ni kutambuliwa, kusikilizwa na kupewa mazingira yanayotuongezea uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Dk. Msigwa huku akipigiwa makofi na washiriki wa mkutano huo.
Alifafanua kuwa kwa miaka mingi shule binafsi zimeendelea kusaidia serikali kwa kuwekeza mabilioni ya fedha katika majengo, vifaa vya kufundishia, ajira za walimu na huduma nyingine muhimu zinazosaidia kupanua upatikanaji wa elimu nchini.
Akijibu hoja hizo, mgeni rasmi ambaye ni Afisa Taaluma Mkoa wa Iringa, Reginald Msendekwa, alisema serikali inatambua kwa dhati mchango wa sekta binafsi na kwamba wawekezaji wa elimu ni sehemu muhimu ya mfumo wa maendeleo ya taifa.
Msendekwa alisema umoja wa wadau wa elimu unapaswa kuendelea kuimarishwa kwa kuwa taifa linakabiliwa na jukumu kubwa la kupokea wanafunzi wengi zaidi wanaotarajiwa kuingia elimu ya sekondari ifikapo mwaka 2028, hali itakayohitaji nguvu za pamoja kati ya serikali na sekta binafsi.
Alihimiza wadau kuunga mkono utekelezaji wa elimu ya amali, kuimarisha ushirikiano kati ya shule, walimu na wazazi, huku akitoa wito kwa TAMONGSCO kuwasilisha changamoto zake kwa maandishi ili zipatiwe ufumbuzi.
Mkutano huo umeacha ujumbe mzito kuwa safari ya kuijenga Tanzania yenye elimu bora, ushindani wa kimataifa na maendeleo endelevu haitafanikiwa kwa mgawanyiko, bali kwa ushirikiano unaomweka mwanafunzi katikati ya kila maamuzi.
Picha za matukio mbalimbali wakati kikao hicho kikiendelea mkoani Iringa





0 Comments