Kamishna wa skauti Mkoa wa Tanga Dkt Frank Mhilu, akikabidhi zawadi ya Taa kwa Kamishna Mkuu Msaidizi wa Watu wazima wa Skauti na Mafunzo, Abdallah Athumani Sakasa.
.........................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
Katika kipindi ambacho jamii inakabiliwa na changamoto za mmomonyoko wa maadili, Chama cha Skauti Tanzania kimewataka walimu wake kuwa nguzo ya malezi bora ya vijana kwa kuwajengea uzalendo, uadilifu na utayari wa kulinda amani na kutetea taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya walimu wa Skauti yaliyofanyika mkoani Tanga, Kamishna Mkuu Msaidizi wa Watu Wazima wa Skauti na Mafunzo, Abdallah Athumani Sakasa alisema mafunzo hayo yalihusisha kozi za Preliminary Training Course (PTC) na Wood Badge Course.
Sakasa alisema mafunzo ya awali ya PTC yalikuwa na washiriki 29, huku mafunzo ya Wood Badge, ambayo ni ngazi ya pili ya nishani ya uskauti, yakihusisha skauti 20.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa watu wazima watakaosimamia programu za vijana, kwa kuwa jukumu kuu la Chama cha Skauti ni kuwalea watoto na vijana kwa kuwafundisha uzalendo, kudumisha amani na kuwa tayari kulinda na kutetea nchi.
Alifafanua kuwa mafunzo ya Wood Badge yalifanyika kwa siku nane, huku yale ya PTC yakidumu kwa siku nne, yakilenga kuwawezesha washiriki kwenda kuwalea watoto katika maeneo yote Mkoani Tanga.
Amewataka wahitimu hao kwenda kuendeleza elimu ya uadilifu na maadili, akisisitiza kuwa Chama cha Skauti kimeendelea kujipambanua kwa kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Kwa upande wake, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Tanga, Dkt. Frank Mhilu, alisema mafunzo hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Galanos yamewezesha kupatikana kwa wakufunzi zaidi ya 20.
Aliwasihi wahitimu kuwa walimu bora wa Skauti kwa kuelimisha kwa weledi, kuishi maisha ya uadilifu na kuzingatia taratibu za chama.
"Tulichojifunza kikawe mwanga wa kuendesha mambo yetu kwa taratibu husika," alisema Dkt. Mhilu.
Akizungumzia mmomonyoko wa maadili, Dkt. Mhilu alisema changamoto hiyo imeongezeka kupitia matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii, hivyo akawataka wahitimu kuwalea watoto na vijana katika maadili mema huku wakiwafundisha matumizi sahihi ya teknolojia.
"Kuna mengi yanayofanyika kupitia mitandao ya kijamii ambayo siyo mazuri na ni wajibu wetu kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, si tu kwa kupata elimu bali pia kujifunza uadilifu," alisema Dkt Mhilu.
Aidha Dkt Mhilu aliwataka wahitimu kuwa mstari wa mbele kukemea viashiria vya migogoro vinavyojitokeza katika maeneo yao ya kazi, akisema kufanya hivyo kutusaidia kuimarisha vhama chao.
Pia alisisitiza umuhimu wa walimu wa Skauti kuonyesha uadilifu katika matendo na tabia zao kwa wanafunzi, jambo litakalosaidia kujenga nidhamu na kuendelea kuheshimika miongoni mwa jamii.
Dkt. Mhilu aliwakumbusha wanachama wa Skauti umuhimu wa kulipa ada pamoja na kusajili makundi yao kwa wakati.
Naye Kamishna wa Skauti Wilaya ya Tanga, Rahim Ibrahim, alisema washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Ibrahim, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kambi ya Galanos, alisema washiriki walifanya usafi katika Zahanati ya Amboni, Ofisi ya Mtendaji wa Amboni na uwanja wa mikutano wa Mabokweni.
Alisema matarajio ya Chama cha Skauti ni kuona wahitimu wanatumia maarifa waliyopata kuelimisha jamii na kuchangia kulinda na kudumisha mila na desturi za watanzania.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya Wood Badge, Catherine Mapunda, alisema amefarijika kujifunza mbinu mbalimbali za kuwalea vijana katika maadili na usalama na hivyo kudumisha amani.
"Kupitia mafunzo haya tumejifunza mambo mengi yatakayotusaidia katika kuwalea vyema vijana wetu kimaadili, tutahakikisha wanakuwa wazalendo na watetezi kwa nchi yao," alisema Catherine.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Watu Wazima wa Skauti na Mafunzo, Abdallah Sakasa, akizungumza wakati wa ufungaji Kambi ya Mafunzo mkoani Tanga.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Watu Wazima wa Skauti na Mafunzo, Abdallah Sakasa akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa kozi za mafunzo ya uongozi kwa skauti baada ya kuhitimu.










No comments:
Post a Comment