Wamshukuru Rais Samia kwa mazingira ya utulivu
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msambweni, Jijini Tanga, Alphonce Denis Mboya.
..............................................................
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAKATI maeneo mbalimbali nchini yakifuatilia kwa karibu hali ya usalama kutokana na taarifa za tishio la maandamano la Julai 7, Mkoa wa Tanga umeendelea kuwa tulivu huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku.
Hali hiyo imeendelea kudhihirisha thamani ya amani katika kujenga uchumi na ustawi wa jamii.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msambweni, Jijini Tanga, Alphonce Denis Mboya, ambaye pia ni Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na mfanyabiashara, amesema wananchi wa Tanga wameamua kuenzi amani kwa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu.
Amesema tangu asubuhi ya Julai 7 wafanyabiashara waliendelea kufungua maduka yao kama kawaida, huku wananchi wakiendelea na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Mboya, ambaye anamiliki duka la vifaa vya ujenzi (hardware) na duka la nguo katika eneo la Ngamiani katikati ya Jiji la Tanga, amesema hali ilikuwa shwari siku nzima.
Kwa mujibu wa Mboya, mwitikio huo unaonyesha namna wananchi wa Tanga walivyo karibu na Serikali yao katika kulinda na kudumisha amani, jambo lililowapa nafasi ya kuendelea na shughuli za maendeleo bila kuwepo na hofu.
Amesema wananchi pia wameendelea kuthamini juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuupa Mkoa wa Tanga kipaumbele katika kuimarisha uchumi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, hatua ambayo imeanza kuleta matokeo chanya.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msambweni, Jijini Tanga, Alphonce Denis Mboya, ambaye pia ni Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara.
.......................................................
Mboya amesema vurugu hazina manufaa kwa maendeleo ya wananchi badala yake, amesisitiza kuwa pale kunapokuwa na changamoto au kero, ni vyema zifikishwe kwa mamlaka husika, ikiwemo kwa njia ya maandishi, ili ziweze jupatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Aidha, amesema wafanyabiashara wa Tanga kupitia vikao vyao mbalimbali wameonesha msimamo wa kutokukubali vitendo vya vurugu, wakieleza kuwa wanahitaji mazingira salama yatakayowawezesha kufanya biashara na kuinua uchumi wao.
"Tanzania kwa mazuri yote ni upendo wa Mungu kwa watu wake, ndiyo maana amani imetamalaki kwa miaka mingi. Tuendelee kushirikiana na Serikali yetu ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi kikamilifu," alisema Mboya.
Ameongeza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na imekuwa ikitoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha changamoto zao kupitia mamlaka husika, badala ya kuchukua njia zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu nchini
Pamoja na hayo, Mboya ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuharakisha kukamilisha ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani, akisema mradi huo unasubiriwa kwa hamu na wananchi kutokana na matarajio makubwa ya kufungua fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Amesema kwamba, wananchi wengi wanaamini kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za maendeleo kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Msambweni, Jijini Tanga, Alphonce Denis Mboya, ambaye pia ni Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara.












No comments:
Post a Comment