Viongozi wa Kampuni za Emirates Leisure Retail Zanzibar (ELR), DNATA, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Fukuchani wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara ya kielimu walioifanya Juni 30, 2026 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume jikiwa moja la tukio katika Kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
..............................
Na Mwandishi
Wetu, Zanzibar
KATIKA kuadhimisha
Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila mwaka Juni 16, Kampuni ya Emirates
Leisure Retail Zanzibar (ELR), kwa kushirikiana na Kampuni ya DNATA na Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), wamefanikisha ziara ya kielimu kwa
wanafunzi 50 pamoja na walimu watatu wa Shule ya Msingi Fukuchani iliofanywa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Ziara hiyo
ililenga kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu huduma
mbalimbali zinazotolewa katika uwanja wa ndege, ikiwemo huduma za abiria,
usalama wa viwanja vya ndege, pamoja na kuwafahamisha kuhusu fursa mbalimbali
za ajira na taaluma katika sekta ya usafiri wa anga.
Akizungumza katika
ziara hiyo, Mratibu wa ziara hiyo ambaye pia ni Afisa Utawala Msaidizi wa
Emirates Leisure Retail Zanzibar, Hussein Ramadhani Layya (Msokolo), alisema
kuwa maadhimisho hayo yalikuwa na lengo la kuwapa watoto elimu, motisha na
uzoefu wa vitendo unaoweza kuwasaidia kufikia ndoto zao za baadaye.
"Ni faraja kubwa kuona tabasamu na furaha za watoto hawa. Tunaamini kuwa kuwapatia nafasi ya kujifunza nje ya darasa kunawajengea uelewa mpana, kujiamini na kuwahamasisha kufikia ndoto zao. Kama kampuni, tunaamini kuwa watoto ni hazina ya taifa, hivyo kuwekeza katika elimu na maendeleo yao ni kuwekeza katika mustakabali wa Zanzibar na Afrika kwa ujumla," alisema Layya.
Kwa upande
wao, viongozi wa Emirates Leisure Retail Zanzibar (ELR) na DNAATA walisema kuwa
kampuni hizo zitaendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii kupitia programu
mbalimbali zinazolenga kuimarisha elimu, afya na ustawi wa jamii.
Viongozi hao
kwa nyakaati tofaauti walieleza kuwa shughuli hizo ni sehemu ya utamaduni wa
kampuni hizo wa kurejesha kwa jamii na kuunga mkono juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha elimu, malezi na ustawi wa watoto.
Aidha, viongozi
hao walisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za umma una
mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye elimu bora na fursa sawa kwa watoto
wote.
Viongozi hao
waliahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza miradi
yenye manufaa kwa jamii.
Mbali na
ziara ya kielimu, Emirates Leisure Retail Zanzibar (ELR) na DNATA waliwezesha ziara
hiyo kwa kutoa usafiri, chakula na zawadi mbalimbali kwa wanafunzi ili
kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo. Hatua hiyo
ilihakikisha watoto wote walipata fursa ya kujifunza, kula na kufurahia siku
hiyo katika mazingira ya upendo, mshikamano na kujali.
Shughuli
hiyo ilionesha dhamira ya kampuni hizo ya kuendelea kutekeleza programu za
uwajibikaji kwa jamii (CSR), sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha elimu, malezi bora na ustawi wa watoto.
ELR na DNATA zimesisitiza kuwa zitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali
katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa jamii na kuchangia maendeleo
endelevu ya Zanzibar.
Shukrani maalumu zilitolewa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), uongozi wa Shule ya Msingi Fukuchani, walimu, wazazi na wadau wote waliochangia kufanikisha ziara hiyo ya kielimu.
Ziara hiyo
ilihitimishwa kwa wanafunzi kutembelea maeneo mbalimbali ya Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ambapo walipata mafunzo na maelezo kutoka kwa
wataalamu wa sekta ya usafiri wa anga kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanyika
uwanjani. Wanafunzi walijifunza kwa vitendo namna uwanja wa ndege unavyofanya
kazi na umuhimu wa kila idara katika kuhakikisha usalama na utoaji wa huduma
bora kwa wasafiri.
Maadhimisho hayo yalimalizika kwa watoto kurejea shuleni wakiwa na furaha, maarifa mapya na hamasa ya kuendelea kujifunza kwa bidii ili kutimiza ndoto zao za baadaye. Tukio hilo limeendelea kudhihirisha dhamira ya Emirates Leisure Retail Zanzibar (ELR), DNATA na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) ya kuwekeza katika elimu, malezi na ustawi wa watoto kupitia ushirikiano imara na jamii, kwa kuamini kuwa watoto wa leo ndio viongozi na wataalamu wa kesho.
KUHUSU SIKU
YA MTOTO WA AFRIKA: HISTORIA YA APARTHEID, VIONGOZI WA UKOMBOZI WA AFRIKA NA
WITO WA KUPINGA XENOPHOBIA
Kila mwaka
tarehe 16 Juni, Bara la Afrika huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, siku muhimu
ya kumbukumbu, elimu na tafakuri kuhusu haki za watoto na historia ya mapambano
ya Waafrika dhidi ya ubaguzi na ukandamizaji.
Siku hii
ilianzishwa rasmi mwaka 1991 na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa
ni Umoja wa Afrika (AU), ikiwa ni heshima kwa watoto waliopoteza maisha katika
maandamano ya Soweto nchini Afrika Kusini mwaka 1976.
1. HISTORIA
YA SOWETO NA APARTHEID
Mnamo tarehe
16 Juni 1976, maelfu ya wanafunzi wa Soweto waliandamana kwa amani wakipinga
mfumo wa Apartheid, ambao uliwabagua Waafrika kwa misingi ya rangi na kuwanyima
haki za msingi.
Wanafunzi
hao walipinga uamuzi wa serikali uliowalazimisha kutumia lugha ya Kiafrikaans
kama lugha ya kufundishia, wakidai elimu bora, usawa na heshima kwa utu wao.
Badala ya
kusikilizwa, polisi wa serikali ya Apartheid waliwavamia kwa risasi na mabomu
ya machozi. Watoto wengi waliuawa, kujeruhiwa na wengine kukamatwa. Tukio hilo
liliibua hasira na huruma duniani na kuwa alama ya mapambano ya haki za
binadamu.
2. VIONGOZI
WA UKOMBOZI WA AFRIKA
Mapambano
dhidi ya ukoloni na ubaguzi hayakuishia Afrika Kusini pekee, bali yalienea
katika bara lote la Afrika. Viongozi mbalimbali walijitokeza kuongoza harakati
za ukombozi, miongoni mwao wakiwa:
Kwame
Nkrumah – Ghana
Julius
Nyerere – Tanzania
Jomo
Kenyatta – Kenya
Patrice
Lumumba – DR Congo
Ahmed Sékou
Touré – Guinea
Samora
Machel – Msumbiji
Agostinho
Neto – Angola
Amílcar
Cabral
Kenneth
Kaunda – Zambia
Robert
Mugabe – Zimbabwe
Joshua Nkomo
– Zimbabwe
Sam Nujoma –
Namibia
Nelson
Mandela – Afrika Kusini
Oliver Tambo
– Afrika Kusini
Walter
Sisulu – Afrika Kusini
Steve Biko –
Afrika Kusini
Desmond Tutu
– Afrika Kusini
Thomas
Sankara – Burkina Faso
Haile Selassie
– Ethiopia
Viongozi
hawa walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi na kuimarisha
mshikamano wa Waafrika kupitia dhana ya Pan-Africanism.
3. ELIMU,
UKOMBOZI NA USTAWI WA MTOTO
Leo hii,
Siku ya Mtoto wa Afrika imekuwa zaidi ya kumbukumbu ya historia. Ni siku ya
kuwakumbusha viongozi, jamii na taasisi zote kwamba watoto wanahitaji:
Elimu bora
na jumuishi
Huduma za
afya na lishe
Ulinzi dhidi
ya ukatili na unyanyasaji
Mazingira
salama ya kukua na kujifunza
Haki ya
kushiriki katika maamuzi yanayowahusu
Katika
kuadhimisha siku hiyo, Emirates Leisure Retail Zanzibar (ELR) kwa kushirikiana
na dnata na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) waliandaa ziara ya
kielimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Fukuchani katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Ziara hiyo
iliwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu huduma za usafiri wa
anga, usalama wa viwanja vya ndege na fursa za ajira katika sekta hiyo.
Kwa mujibu
wa waandaaji, imekuwa ni utamaduni wa ELR na dnata kushirikiana na jamii
kupitia programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zinazolenga kuimarisha elimu,
afya na ustawi wa jamii.
4. WITO
DHIDI YA XENOPHOBIA
Licha ya
ushindi dhidi ya Apartheid, Afrika Kusini bado inakabiliwa na changamoto ya
xenophobia, yaani chuki dhidi ya wageni kutoka mataifa mengine ya Afrika.
Sababu zake
ni pamoja na ukosefu wa ajira, umasikini, ushindani wa rasilimali na taarifa za
upotoshaji. Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa wakati wa mapambano ya uhuru,
mataifa mengi ya Afrika yaliwapa hifadhi na msaada wapigania uhuru wa Afrika
Kusini.
Hivyo basi,
xenophobia inapingana na historia ya mshikamano wa Waafrika na inapaswa
kulaaniwa na kila mwenye nia ya kuona Afrika yenye amani na umoja.
HITIMISHO
Siku ya
Mtoto wa Afrika ni zaidi ya kumbukumbu ya kihistoria. Ni somo kwa jamii kwamba
uhuru, haki na maendeleo haviji bila mshikamano.
Kwa kuenzi watoto wa Soweto, kuwaheshimu viongozi wa ukombozi wa Afrika na kupinga ubaguzi wa aina yoyote, tunaweza kujenga Afrika yenye amani, usawa na matumaini kwa vizazi vijavyo.
Picha ya paamoja wakati wa ziara hiyo.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.















No comments:
Post a Comment