𝐓𝐔𝐌𝐄 𝐘𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐘𝐀 𝐔𝐍𝐄𝐒𝐂𝐎 𝐘𝐀𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈 𝐔𝐙𝐈𝐍𝐃𝐔𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐖𝐎𝐍𝐆𝐎𝐙𝐎 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐖𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐀𝐍𝐎 𝐊𝐀𝐓𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐙𝐀𝐙𝐈 𝐍𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐙𝐀𝐍𝐙𝐈𝐁𝐀𝐑 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, September 4, 2026

𝐓𝐔𝐌𝐄 𝐘𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐘𝐀 𝐔𝐍𝐄𝐒𝐂𝐎 𝐘𝐀𝐒𝐇𝐈𝐑𝐈𝐊𝐈 𝐔𝐙𝐈𝐍𝐃𝐔𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐖𝐎𝐍𝐆𝐎𝐙𝐎 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐖𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐀𝐍𝐎 𝐊𝐀𝐓𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐙𝐀𝐙𝐈 𝐍𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐙𝐀𝐍𝐙𝐈𝐁𝐀𝐑

ZANZIBAR, Septemba 3, 2026 — Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania imeshiriki katika uzinduzi wa Mwongozo wa Mawasiliano kati ya Mzazi na Mtoto kuhusu Haki ya Afya ya Uzazi (Parent-Child Communication – PCC Toolkit), unaolenga kuimarisha mawasiliano ndani ya familia na kusaidia kulinda afya na ustawi wa watoto na vijana Zanzibar.

Mwongozo huo unazinduliwa leo katika Hoteli ya Verde Zanzibar na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mheshimiwa Zawadi Amour Nassor, katika hafla iliyowakutanisha viongozi na wadau mbalimbali wanaohusika na afya, ulinzi na ustawi wa watoto.

Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar na UNESCO, ukiwa na lengo la kuwasaidia wazazi na walezi ku

anzisha mazungumzo sahihi na yenye kujenga na watoto kuhusu afya ya uzazi, mabadiliko ya ukuaji, usalama na namna ya kujilinda dhidi ya mazingira yanayoweza kuhatarisha afya na ustawi wao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Zawadi anasema Serikali ya Zanzibar imejizatiti kuhakikisha watoto wanakulia katika mazingira salama, wanasikilizwa na hawabaki nyuma, akisisitiza kuwa malezi na ulinzi wa mtoto ni jukumu la pamoja.

Anasema afya ya uzazi ni sehemu ya afya na ustawi wa mtoto, hivyo wazazi, walezi, taasisi na jamii wanapaswa kushirikiana katika kuwapatia watoto taarifa sahihi na mazingira yanayowawezesha kukua kwa usalama.
“Mtoto ni kama mbegu; ukimlea vizuri atakuwa na afya bora,” anasema.

Naibu Waziri pia anawataka wadau kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazochangia ukatili na udhalilishaji wa watoto, akisisitiza umuhimu wa kuzuia matukio hayo kabla hayajatokea.

Anasema changamoto hizo zinahitaji ushirikiano wa karibu baina ya taasisi, jamii na wadau mbalimbali, huku akigusia pia umuhimu wa wanaume kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

“Tuzuie matukio yanayosababisha udhalilishaji ili tuweze kupata taifa bora,” anasisitiza.

Kwa upande wa UNESCO, Mr Mathias Luhanya, National Project Officer, anasema mwongozo huo umefanyiwa kazi tangu mwaka 2020, na kufikia hatua ya kuzinduliwa rasmi ni matokeo ya uvumilivu, juhudi na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Anasema mwongozo huo unalenga kumsaidia mzazi kuelewa namna bora ya kuzungumza na mtoto kuhusu afya ya uzazi, kumsaidia kuelewa mabadiliko anayopitia na kutambua mazingira yanayoweza kuhatarisha afya na usalama wake.

Ushiriki wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania katika uzinduzi huo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya UNESCO, Serikali ya Zanzibar na wadau wa kitaifa katika kuendeleza programu zinazolenga elimu, afya, ulinzi na ustawi wa watoto na vijana.

Hatua hiyo pia inaendana na juhudi za UNESCO za kuwawezesha watoto na vijana kupata maarifa na mazingira salama yanayowasaidia kulinda afya zao na kufikia uwezo wao.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mheshimiwa Zawadi anaishukuru UNESCO kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kufanikisha uzinduzi wa mwongozo huo, akisisitiza kuwa mafanikio katika kumlinda mtoto yanahitaji dhamira na ushirikiano wa pamoja.

“Penye nia pana njia.”

Uzinduzi wa mwongozo huo unaweka msisitizo kwamba kumlinda mtoto ni jukumu la pamoja la mzazi, familia, jamii, Serikali, taasisi na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, wanasikilizwa na wanapata fursa ya kuwa na afya bora na maisha yenye ustawi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad