𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐇𝐀𝐌𝐔 𝐖𝐀 𝐏𝐀𝐌𝐎𝐉𝐀 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐃𝐇𝐀𝐍𝐀 𝐘𝐀 𝐔𝐆𝐀𝐓𝐔𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐃𝐀𝐑𝐀𝐊𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐌𝐋𝐀𝐊𝐀 𝐙𝐀 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐙𝐀 𝐌𝐈𝐓𝐀𝐀 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, September 4, 2026

𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐇𝐀𝐌𝐔 𝐖𝐀 𝐏𝐀𝐌𝐎𝐉𝐀 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐃𝐇𝐀𝐍𝐀 𝐘𝐀 𝐔𝐆𝐀𝐓𝐔𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐃𝐀𝐑𝐀𝐊𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐌𝐋𝐀𝐊𝐀 𝐙𝐀 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐙𝐀 𝐌𝐈𝐓𝐀𝐀

Serikali imesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu dhana ya ugatuzi wa madaraka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo, tarehe 3 Septemba 2026, na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, wakati wa ufunguzi wa Kikao Maalum cha Kujenga Uelewa wa Pamoja kwa Wakurugenzi wa Sera na Mipango kuhusu dhana ya Ugatuzi, kinachofanyika Morogoro kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Ndugu Adolf H. Ndunguru.

Alisema ugatuzi si ajenda mpya nchini, bali umekuwa ukitekelezwa kwa muda mrefu kupitia mageuzi ya Serikali za Mitaa, hususan Tamko la Kisera kuhusu Maboresho ya Serikali za Mitaa la mwaka 1998, lililoanzisha msingi wa utekelezaji wa Ugatuzi wa Madaraka (Decentralisation by Devolution – D-by-D).

Aidha, Dkt. Mussa alieleza kuwa lengo kuu la ugatuzi ni kusogeza mamlaka, majukumu na rasilimali karibu na wananchi, ili maamuzi yafanyike katika ngazi zinazofaa na huduma zitolewe kwa ufanisi zaidi.

Dkt. Mussa aliongeza kuwa, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na ugatuzi, bado kumekuwa na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa. Miongoni mwa changamoto hizo ni uwezo mdogo wa baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, utegemezi mkubwa wa fedha kutoka Serikali Kuu na kurejeshwa kwa baadhi ya majukumu katika usimamizi wa sekta, hali inayoweza kupunguza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma.

Awali, akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Bw. John Cheyo, alisema kikao hicho ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, aliyeelekeza kufanyika kwa mafunzo kwa ajili ya kupata uelewa wa dhana ya ugatuzi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad