𝐊𝐈𝐓𝐔𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐅𝐎𝐑𝐎𝐃𝐇𝐀 𝐊𝐔𝐀𝐍𝐙𝐈𝐒𝐇𝐖𝐀 𝐋𝐎𝐋𝐈𝐎𝐍𝐃𝐎 𝐍𝐀 𝐒𝐀𝐋𝐄 𝐄𝐍𝐃𝐀𝐏𝐎 𝐕𝐈𝐆𝐄𝐙𝐎 𝐕𝐈𝐓𝐀𝐓𝐈𝐌𝐈𝐀 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, September 5, 2026

𝐊𝐈𝐓𝐔𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐅𝐎𝐑𝐎𝐃𝐇𝐀 𝐊𝐔𝐀𝐍𝐙𝐈𝐒𝐇𝐖𝐀 𝐋𝐎𝐋𝐈𝐎𝐍𝐃𝐎 𝐍𝐀 𝐒𝐀𝐋𝐄 𝐄𝐍𝐃𝐀𝐏𝐎 𝐕𝐈𝐆𝐄𝐙𝐎 𝐕𝐈𝐓𝐀𝐓𝐈𝐌𝐈𝐀

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga Kituo au Vituo vya Forodha katika maeneo ya mpakani ya Tarafa za Loliondo na Sale, Wilaya ya Ngorongoro.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha-Dodoma)

*************

Na Peter Haule, WF, Dodoma

Serikali imesema itaanzisha Kituo cha Forodha katika maeneo ya mpakani ya Tarafa za Loliondo na Sale, Mkoani Arusha, baada ya kukamilika kwa tathmini na endapo maeneo hayo yatakuwa yamekidhi vigezo vilivyowekwa.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga Kituo au Vituo vya Forodha katika maeneo ya mpakani ya Tarafa za Loliondo na Sale, Wilaya ya Ngorongoro.

Mhe. Munde alisema vigezo vinavyotumika katika kuanzisha vituo vya Forodha ni pamoja na hali halisi ya mpaka (strategic nature), idadi ya watu wanaoishi katika eneo husika la mpaka na kiasi cha mizigo kinachohudumiwa.

“Serikali iliweka vigezo mahususi vinavyozingatiwa kabla ya kuanzisha vituo vya Forodha mipakani ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuhakikisha ufanisi wa vituo husika,” alisema Mhe. Munde.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa huduma za forodha katika maeneo ya mipakani, ikiwemo maeneo ya Tarafa za Loliondo na Sale, kwa kuwa huduma hizo zinaweza kurahisisha biashara, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuimarisha udhibiti wa biashara zinazovuka mipaka.

Aidha, Mhe. Munde alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na usimamizi wa mipaka, itafanya tathmini ya mahitaji ya kuanzisha Kituo cha Forodha katika maeneo hayo kwa kuzingatia vigezo mahususi vilivyoainishwa.

Alisema baada ya kukamilika kwa tathmini na endapo itaonekana kuwa kuna umuhimu wa kuanzisha vituo hivyo, Serikali itajumuisha mradi huo katika mipango na bajeti zake kulingana na vipaumbele vya Taifa.

Serikali pia itaendelea kuhakikisha kuwa huduma za kiforodha zinawafikia wananchi na wafanyabiashara kwa ukaribu zaidi, ili kurahisisha biashara na kudhibiti biashara ya magendo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad