𝐖𝐈𝐙𝐀𝐑𝐀 𝐘𝐀 𝐅𝐄𝐃𝐇𝐀, 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀 𝐁𝐀𝐑𝐀 𝐍𝐀 𝐙𝐀𝐍𝐙𝐈𝐁𝐀𝐑 𝐙𝐀𝐁𝐀𝐃𝐈𝐋𝐈𝐒𝐇𝐀𝐍𝐀 𝐔𝐙𝐎𝐄𝐅𝐔 𝐖𝐀 𝐃𝐀𝐅𝐓𝐀𝐑𝐈 𝐋𝐀 𝐊𝐈𝐄𝐋𝐄𝐊𝐓𝐑𝐎𝐍𝐈𝐊𝐈 𝐋𝐀 𝐓𝐀𝐀𝐑𝐈𝐅𝐀 𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐅𝐈𝐒𝐀 𝐔𝐍𝐔𝐍𝐔𝐙𝐈 𝐍𝐀 𝐔𝐆𝐀𝐕𝐈 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈𝐍𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, September 9, 2026

𝐖𝐈𝐙𝐀𝐑𝐀 𝐘𝐀 𝐅𝐄𝐃𝐇𝐀, 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀 𝐁𝐀𝐑𝐀 𝐍𝐀 𝐙𝐀𝐍𝐙𝐈𝐁𝐀𝐑 𝐙𝐀𝐁𝐀𝐃𝐈𝐋𝐈𝐒𝐇𝐀𝐍𝐀 𝐔𝐙𝐎𝐄𝐅𝐔 𝐖𝐀 𝐃𝐀𝐅𝐓𝐀𝐑𝐈 𝐋𝐀 𝐊𝐈𝐄𝐋𝐄𝐊𝐓𝐑𝐎𝐍𝐈𝐊𝐈 𝐋𝐀 𝐓𝐀𝐀𝐑𝐈𝐅𝐀 𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐀𝐅𝐈𝐒𝐀 𝐔𝐍𝐔𝐍𝐔𝐙𝐈 𝐍𝐀 𝐔𝐆𝐀𝐕𝐈 𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈𝐍𝐈

Maafisa Ugavi Wandamizi kutoka Wizara za Fedha za Tanzania Bara na Zanzibar, wakifuatilia kwa umakini mafunzo kuhusu Mfumo wa Taarifa za Maafisa Ununuzi na Ugavi, yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma.
Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, akiagana na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Sera za Ununuzi Zanzibar, Bi. Asma Mohamed, baada ya kukamilika kwa mafunzo kuhusu Mfumo wa Taarifa za Maafisa Ununuzi na Ugavi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma. 
------------------------------------

Na Martha Mbena na Jordan Mbwambo, WF, Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma na wa Wizara ya Fedha na Mipango, Zanzibar, Idara ya Usimamizi Sera za Umma, wamebadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya Daftari la Kielektroniki la Taarifa za Maafisa Ununuzi na Ugavi Serikalini.

Watumishi hao wamekutana jijini Dodoma kwa ajili ya kujifunza namna ya usanifu na ujenzi wa  Daftari la Kielektroniki la Taarifa za Maafisa Ununuzi na Ugavi Serikalini (Procurement and Supplies Personnel Information System – PSPIS) ambalo hutumika kama zana ya utekelezaji wa matakwa ya Kifungu  cha  7(j) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023, kinachoipa Wizara jukumu la kushauri kuhusu muundo, uteuzi wa Wakuu wa Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi, na kupendekeza uhamisho wa watumishi wa ununuzi na ugavi.

Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho, Kaimu Kamishna wa Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, amesema kuwa Mfumo wa PSPIS ni nyenzo muhimu inayosaidia Serikali kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotekeleza majukumu ya ununuzi wa umma na ugavi.

“Matumizi ya Mfumo huo yanawezesha taarifa za maafisa wa ununuzi na ugavi kukusanywa na kusimamiwa kwa ufanisi, hatua inayosaidia Serikali kufanya maamuzi kwa kuzingatia taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati,” amesema Bw. Haraba.

Amesema taarifa hizo ni muhimu katika kupanga rasilimali watu, kutambua mahitaji ya kada, kujenga uwezo wa watumishi na kutoa ushauri wa kisera na kiutendaji.

Aidha, daftari la watumishi wanaofanya kazi za ununuzi na ugavi katika Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi (PMUs) ni nyenzo ya kiutawala inayolenga kuiwezesha Serikali kuwa na kumbukumbu sahihi, zilizohakikiwa na zinazosasishwa kuhusu watumishi hao.

Pia, katika kikao kazi hicho, wataalamu wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Kifedha na huduma za ndani, Wizara ya Fedha, walitoa maelezo kuhusu matumizi ya Mfumo wa PSPIS na namna ulivyounganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) kama mbinu ya kuhakikisha mifumo hii inabadilishana taarifa kwa usahihi.

 

Kikao kazi hicho kimekuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu na maarifa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika usimamizi wa Kada ya Ununuzi wa Umma na Ugavi, pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kuboresha utendaji wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad