----------------------
Serikali imewekeza jumla ya Shilingi bilioni 67.9 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Katika eneo la wanafunzi, Prof. Pallangyo amesema idadi imeongezeka kutoka wanafunzi 24,494 mwaka 2022 hadi 37,397 mwaka huu wa taaluma, sawa na ongezeko la asilimia 52.7.
Ameongeza kuwa kati ya wanafunzi hao, 19,342 ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka HESLB, sawa na asilimia 51.7, huku wanafunzi 137 wa Kampasi ya Zanzibar wakinufaika na mikopo kutoka Zanzibar Higher Education Students’ Loan Board.
Aidha amebainisha kuwa TIA imeongeza programu za mafunzo kutoka 49 mwaka 2022 hadi 54, zikiwemo Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano, TIA imekuwa na wahitimu wapatao 62,680, huku taasisi hiyo ikiendelea kuimarisha uwezo wa watumishi ambapo kwa sasa ina maprofesa tisa. Watumishi 78 wamefadhiliwa kwa ajili ya masomo ya shahada za juu, kati yao 48 wamehitimu na 30 wanaendelea na masomo ya PhD.
Ameongeza kuwa TIA imepanua pia upatikanaji wa programu za shahada ya uzamili kutoka Kampasi ya Dar es Salaam pekee hadi Kampasi za Zanzibar, Mbeya na Singida, huku Kampasi ya Mwanza ikitoa fursa hiyo kuanzia mwaka huu.












No comments:
Post a Comment