𝐌𝐀𝐒𝐀𝐔𝐍𝐈 𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐓𝐔𝐌𝐈𝐙𝐈 𝐘𝐀 𝐓𝐄𝐊𝐍𝐎𝐋𝐎𝐉𝐈𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈 𝐖𝐀 𝐁𝐔𝐋𝐔𝐔 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, September 7, 2026

𝐌𝐀𝐒𝐀𝐔𝐍𝐈 𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐓𝐔𝐌𝐈𝐙𝐈 𝐘𝐀 𝐓𝐄𝐊𝐍𝐎𝐋𝐎𝐉𝐈𝐀 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈 𝐖𝐀 𝐁𝐔𝐋𝐔𝐔

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiingia Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam kufungua Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) unaofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akifungua Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) unaofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) unaofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile wakati akiingia Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam kufungua Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) unaofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026. Aliyesimama katikati ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rasi Dkt. Richard Muyungi.
-----------------

Na; Mwandishi Wetu -Dar es Saalam

Serikali inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za dijitali, mifumo ya kisasa ya usimamizi wa bandari na biashara, pamoja na matumizi ya taarifa za kisayansi katika kufanya maamuzi ya kutambua kuwa Uchumi wa Buluu wa kisasa unahitaji wataalamu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia mpya.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo kwa niaba ya Mhe. Deogratius Ndejembi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufunguzi wa Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu (IBEC) unaofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam.


Amesema ni wajibu kuendelea kushirikiana katika tafiti za kisayansi, uhamishaji wa teknolojia rafiki, uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu, usimamizi wa rasilimali za pamoja na ulinzi wa mazingira ya bahari ili kuhakikisha tunanufaisha kizazi cha sasa na kijcho.


“Kongamano hili linafanyika katika kipindi muafaka ambapo dunia na hasa bara la Afrika limeendelea kutambua kuwa bahari, maziwa, mito, maji chini ya ardhi na maeneo ya pwani si tu urithi wa asili, bali ni rasilimali za kimkakati zinazochangia usalama wa chakula, biashara, uwekezaji, ajira, na ustawi wa jamii kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.


“Kauli mbiu ya kongamano hili isemayo “Powering Blue Initiatives for Sustainable Economic Growth in Africa” inatukumbusha kuwa maendeleo ya Uchumi wa Buluu yanahitaji zaidi ya kuwa na rasilimali; yanahitaji kuziwezesha na kuzibadilisha rasilimali za uchumi wa buluu kuwa fursa halisi za kiuchumi kupitia sayansi, teknolojia, ubunifu, uwekezaji na ushirikiano wa wadau mbalimbali.” Amesema Mhe. Masauni.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema Uchumi wa Buluu ni eneo lenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na rasilimali na fursa zinazopatikana katika bahari, maziwa, mito, maeneo ya pwani na maeneo mengine ya maji


“Kwa mtazamo wa Serikali, Uchumi wa Buluu unapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia misingi ya matumizi endelevu ya rasilimali, usimamizi wa mazingira, kuongeza thamani, kukuza ajira na kipato, kuongeza biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.” Amesema Mhe. Kihenzile.


Aidha Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo amesema Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024, ambayo imeweka msingi wa kitaifa wa kusimamia, kuratibu na kutumia kwa uendelevu fursa zinazopatikana katika rasilimali za maji.


“Tunahitaji maarifa na ujuzi; tunahitaji tafiti na ubunifu; tunahitaji sera na sheria zinazotekelezeka; tunahitaji teknolojia; tunahitaji uwekezaji; na tunahitaji ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad