𝐌𝐅𝐔𝐊𝐎 𝐖𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐈𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐓𝐀𝐅𝐔𝐓𝐀 𝐕𝐘𝐀𝐍𝐙𝐎 𝐌𝐁𝐀𝐃𝐀𝐋𝐀 𝐕𝐘𝐀 𝐅𝐄𝐃𝐇𝐀 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, September 4, 2026

𝐌𝐅𝐔𝐊𝐎 𝐖𝐀 𝐓𝐀𝐈𝐅𝐀 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐈𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐓𝐀𝐅𝐔𝐓𝐀 𝐕𝐘𝐀𝐍𝐙𝐎 𝐌𝐁𝐀𝐃𝐀𝐋𝐀 𝐕𝐘𝐀 𝐅𝐄𝐃𝐇𝐀

Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) umetakiwa kutumia ubunifu kupata vyanzo mbadala vya fedha kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika kikao kazi na watumishi wa NWF jijini Dodoma leo Septemba 4, 2026 amewataka kuwa wabunifu kutafuta vyanzo mbadala vya fedha ili kufanikisha miradi ya maji ya kimkakati ambayo itakuwa kielelezo katika kuchochea maendeleo.

 “Tumefanya vizuri kupitia hati Fungani ya Kijani ya Tanga UWASA sasa ni muda wa kuwa na Hati Fungani ya kifedha inayotolewa kwa ajili ya kugharamamia miradi ya maji” (Water Infrastructure Bond), Waziri Aweso amesema..

Ameitaka Menejimenti ya NWF na watumishi wa taasisi hiyo kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo, ubunifu na uwajibikaji ili kuongeza mchango katika kufanikisha nia ya serikali ya kutoa huduma ya maji iliyo bora, salama, toshelevu na endelevu. 

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri katika kikao hicho amesema ili kuchochea mabadiliko watumishi wa taasisi hiyo wanatakiwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ikiwamo utunzaji wa siri na nyaraka mbalimbali za serikali. 

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maji, Wakili Haji Nandule amesema maelekezo yaliyotolewa katika kikao atahakikisha yanafanyiwa kazi kwa wakati na kusimamia utekelezaji wake.

Mfuko wa Taifa wa Maji ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Maji inayotekeleza Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya 2019, ikikusanya na kusimamia fedha za miradi ya maji, uhifadhi wa vyanzo vya maji na uboreshaji wa huduma ya maji katika jamii nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad