.........................................
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko ya kiutendaji katika ngazi ya makatibu wa mikoa, ambapo kimeteua makaimu makatibu wa mikoa 32 katika mikoa yote ya chama, ambao wataanza kazi mara moja.
Kama sehemu ya maandalizi ya kiutendaji, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, ameitisha semina elekezi ya siku mbili kwa makaimu makatibu hao, itakayofanyika jijini Dodoma kuanzia Septemba 28.
Katika mabadiliko hayo, baadhi ya makatibu wa mikoa na wilaya wamehamishwa, wengine wamepandishwa vyeo kutoka kuwa makatibu wa wilaya hadi makatibu wa mikoa, huku wengine wakistaafu na wengine wakiacha nafasi bila kupangiwa vituo vipya vya kazi.
Miongoni mwa makatibu waliopandishwa cheo ni Twalib Belege, ambaye awali alikuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini na sasa ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga.
Wananchi wa Tanga wanamkaribisha Katibu mpya wa CCM Mkoa wa Tanga, Twalib Belege, katika mkoa huo unaotajwa kuwa lango kuu la uchumi wa Afrika Mashariki.
Wakati wakimkaribisha Katibu mpya, Wanatanga pia wanamuaga aliyekuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, ambaye amemaliza muda wake.
Kizigo anaondoka akiwa ameacha kumbukumbu nzuri kutokana na uongozi wake, huku akitajwa pia kwa ucheshi, upendo na mshikamano aliouonyesha katika kipindi cha uongozi wake.
Aliyekuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, ambaye amemaliza muda wake akisisitiza jambo alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah aliyoifanya Mkata Wilaya ya Handeni Septemba 20, 2026.
Habari hii imeandikwa na Dotto Mwaibale Simu namba 0754362990









No comments:
Post a Comment