Kamanda wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida , Mrakibu Msaidizi Probi Kowinga (kushoto), akitoa taarifa ya tukio hilo Oktoba 21, 2026.
......................
Imeandaliwa na Mtandao wa Singidani Blog
WAPANGAJI wa nyumba moja iliyopo katika Mtaa wa Stendi, mjini Singida, wamenusurika kifo baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto asubuhi ya Oktoba 21, 2026.
Tukio hilo limetokea siku nne tu tangu mtoto mmoja afariki dunia huku watu wazima 41, wakazi wa Unyambwa katika Manispaa ya Singida, wakinusurika kupoteza maisha baada ya kudhaniwa kula makande na kunywa togwa yenye sumu.
Moto huo uliozuka majira ya saa 5:15 asubuhi, ulidhibitiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida, ambalo lilifika eneo la tukio kwa wakati.
Akizungumza eneo la tukio, Kamanda wa Operesheni wa jeshi hilo, Mrakibu Msaidizi Probi Kowinga, alisema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa 5:15 asubuhi na kufika eneo la tukio muda mfupi baadaye, ambapo walikuta moto mkubwa ukiwaka.
Alisema baada ya kufanya uchunguzi wa awali, walibaini kuwa vitu vingi vilivyokuwa vikiungua vilikuwa ni magodoro.
“Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilipambana kadiri lilivyoweza na kufanikiwa kuudhibiti moto huo majira ya saa 6:50 asubuhi,” alisema Kowinga.
Hamisi Ibrahim, ambaye ni mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo na mmiliki wa magodoro yaliyoteketea, alisema nyumba hiyo ilikuwa na wapangaji wanne.
Alisema wapangaji wenzake walikuwa wakiishi katika vyumba vya ndani, huku yeye akiishi vyumba vya nje ambako pia alikuwa akihifadhi magodoro yake ya biashara.
“Wakati tukio la moto lilipotokea sikuwa eneo hilo. Nilipofika baada ya kupigiwa simu, nilikuta magodoro zaidi ya 200 yameteketea kwa moto,” alisema Ibrahim.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Stendi, Theresia Nicodemas, alisema wakati tukio hilo linatokea walikuwa ofisini na waliona moto ukiwaka, hivyo walifika eneo la tukio kujionea hali halisi.
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kuzimia moto katika nyumba zao ili viweze kuwasaidia wakati wa majanga.
“Tunaomba wananchi kuhakikisha wakati wote wanakuwa na vizimia moto katika nyumba zao ili viweze kuwasaidia,” alisema.
Diwani wa Kata ya Ipembe, Omari Hamisi, aliishukuru Serikali kwa kununua vifaa vya kuzimia moto, akisema vimekuwa vikisaidia kukabiliana na majanga ya moto kwa haraka.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stendi, Hussein Amri, alisema hakuwepo eneo la tukio wakati moto huo ulipozuka, lakini aliliomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuhakikisha linafika haraka kila yanapotokea matukio ya aina hiyo.
















No comments:
Post a Comment