Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
Warembo wanaowania taji la Miss Eastern Zone wanatarajiwa kuchuana katika fainali za shindano hilo zitakazofanyika Novemba 6, 2026, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, ambapo mshindi atajinyakulia zawadi ya gari pamoja na tiketi ya kushiriki fainali za Miss Tanzania 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 27, 2026, wilayani Mkuranga, Mkurugenzi wa Miss Eastern Zone, Yusuf Hassan, amesema maandalizi ya shindano hilo yanaendelea na washiriki wanatarajiwa kuingia kambini hivi karibuni katika Kisiwa cha Vikuruti kilichopo Mkuranga.
Amesema warembo hao watasafiri kwa usafiri wa majini kutoka Sea Cliff, Masaki, jijini Dar es Salaam, kuelekea kisiwani humo, huku washiriki wengine wakitarajiwa kupata zawadi mbalimbali.
Hassan amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Idara ya Utamaduni na Michezo, kwa juhudi za kuwezesha vijana kunufaika na mikopo ya makundi maalumu.
Pia amewashukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kwa maelekezo na ushirikiano wao katika kufanikisha maandalizi ya shindano hilo.
Amesema shindano hilo linatarajiwa kunogeshwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwemo D-Voice wa lebo ya WCB, Isha Mashauzi, Yammy Tz na Dogo Parten, pamoja na wasanii wazawa kutoka Mkuranga na Mkoa wa Pwani.
Aidha, amesema mdau mkubwa wa shindano hilo ni BOSS BOSS, huku Adey na wadau wengine wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaounga mkono maandalizi yake.
Kuhusu tiketi, Hassan amesema tayari zimeanza kuuzwa kwa bei ya Sh20,000 kwa tiketi ya kawaida, Sh50,000 kwa VIP na Sh100,000 kwa VVIP.
Amesema tiketi hizo zinapatikana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na ofisi za utamaduni mkoani humo, pamoja na Parachichi, BOSS BOSS Vikindu na Samaki Sport, Morogoro.










No comments:
Post a Comment