TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 28 UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, April 23, 2024

TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 28 UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida , Sifa Mwanjala  akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya kipindi cha Januari hadi Machi 2024.

.......................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog) 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa Sh.Milioni 28. 030 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida , Sifa Mwanjala wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya kipindi cha Januari hadi Machi 2024

Mwanjala alisema kiasi hicho cha fedha kilibainika baada ya kufanya ufuatiliaji wa miradi 11 huku mitano yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.3 ikikutwa na mapungufu mbalimbali. 

Alitaja mapungufu yaliyobainika kuwa ni kufanya malipo ya vifaa vya ujenzi kwa wazabuni yanayohusisha gharama ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) wakati wazabuni hao hawajasajiliwa kwenye mfumo wa walipa kodi wa asilimia 18 hivyo hawakustahili kulipwa fedha hizo, wazabuni kuzidishiwa malipo katika vifaa walivyouza, wazabuni na mafundi kutokukatwa kodi ya zuio pamoja na kutowasilishwa kwa kodi ya zuio TRA. Kutokana na ufuatiliaji huo TAKUKURU iliweza kuokoa kiasi hicho cha fedha. 

Alisema katika ufuatiliaji wa rushwa TAKUKURU walifuatilia utekelezaji wa miradi kumi na moja yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 9.022 katika sekta za Elimu, Ujenzi (Barabaraba) na Afya. miradi hiyo inajumuisha miradi inayotekelezwa ya ujenzi wa vyuo vya ufundi (VETA) na shule za Sekondari za Kutwa katika Kata kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambao unahusisha ujenzi na ukarabati wa Shule za Sekondari, ujenzi wa nyumba za walimu 2 in 1 katika shule za msingi na ujenzi wa vituo vya Afya.

Alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida katika kipindi tajwa ilifanya Warsha tano za kujadili mianya ya rushwa iliyobainika katika chambuzi za mifumo na kuweka mikakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

" Katika warsha hizo changamoto ya kutokatwa kwa kodi ya zuio katika malipo yaliyofanyika kwa vifaa mbalimbali vya ujenzi vilivyonunuliwa ilijadiliwa na mikakati ya kutatua changamoto hiyo iliwekwa ambapo tayari fedha kiasi cha Sh. Milioni 4,8 cha kodi ya zuio kimekatwa na kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya warsha hizo," alisema Mwanjala. 

Mwanjala alisema Ofisi iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 5 na wadau katika Kata 5 ambapo wadau waliibua kero 7. Kero zote 7 zimetatuliwa na taarifa ya utatuzi wa kero hizo imewasilishwa kwa wananchi kupitia vikao.

Alisema kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki, wananchi wa kata ya Kinyeto katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida waliibua kero ya kuuziwa kadi za afya kwa gharama ya Sh 20,000/= wakati wa kupata huduma kwenye kituo cha afya cha Kinyeto. Kero hiyo imetatuliwa na kwa sasa huduma hiyo inapatikana bure. Pia barabara ya Kinyeto ilikuwa inajaa maji na haipitiki imerekebishwa na inapitika.

Alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kero 04 ziliibuliwa zilizohusiana na Kituo cha Afya Kintiku zifuatazo: Kukosekana kwa huduma ya Ex-ray na Ultra sound wakati mashine hizo zipo na hivyo kupelekea wananchi kuifuata huduma hiyo Manyoni. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni (DMO) aliitatua kero hiyo kwa kulipia leseni mamlaka ya mionzi Tanzania na kuomba mtaalam toka Wizara ya Afya ili huduma hiyo iweze kutolewa. 

Akizungumzia kuhusu eneo la elimu kwa umma Mwanjala alisema ofisi iliwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa kwa kufanya yafuatayo:- kutoa elimu kwa waandishi wa habari kuhusu rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, kutoa elimu ya athari za rushwa na dawa za kulevya kwa vijana wa shule za sekondari zipatazo 10 na vyuo 2. 

Pia ofisi ilitoa Semina 40 kwenye makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Umma, Mikutano ya hadhara 16, Maonesho 7, Kutembelea na kuimarisha Klabu za Wapinga Rushwa 73 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo. 

Katika eneo la uchunguzi na mashitaka alisema malalamiko 71 yalipokelewa, ambapo malalamiko 38 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 33 hayakuhusu vitendo vya rushwa. Malalamiko 38 yaliyohusu rushwa, uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na Malalamiko 33 ambayo hayahusiani na rushwa walalamikaji walipewa ushauri. 

Alisema katika kipindi tajwa kesi 5 zilifunguliwa mahakamani, kesi 3 ziliamuliwa ambapo kesi 3 zilishinda na kesi 24 zinaendelea Mahakamani.

 

Alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa robo ya nne ya mwaka 2023/2024 ya kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2024 imeweka Mkakati wa utendaji kazi kwa kufuatilia kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa mkoani hapa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Kuendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya Rushwa hasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao, Kutekeleza  Programu ya TAKUKURU – Rafiki na Kuendelea kutoa elimu ya rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.                                                                                                                                              Alisema TAKUKURU Mkoa wa wa Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya rushwa vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii na hasa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, pia wanatakiwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa   Singida  na Wilaya za Iramba, Ikungi, Mkalama na Manyoni. Kupiga simu ya bure 113 au simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na wakuu wa TAKUKURU wa wilaya kwa namba zifuatazo:

Na

Mkoa /Wilaya

NAMBA YA SIMU

1

RBC – SINGIDA

0738150208

2

DBC - Mkalama

0738150212

3

DBC - Ikungi

0738150213

4

DBC - Iramba

0738150210

5

DBC - Manyoni

0738150211

  

Maafisa wa TAKUKURU Singida wakiwa kwenye mkutano huo wakutoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Taswira ya mkutano huo.
Muonekano wa Jengo la TAKUKURU Mkoa wa Singida.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad