MZEE WA MIAKA 68 AOMBA MSAADA MATIBABU AFANYIWE UPASUAJI TEZI DUME - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, August 12, 2025

MZEE WA MIAKA 68 AOMBA MSAADA MATIBABU AFANYIWE UPASUAJI TEZI DUME

Amesha fanyiwa oparesheni ya kukatwa kidole

Anasubiri kukatwa mguu

Mzee Said Bakari Nyumbu (68) Mkazi wa Mtaa wa Ngurungu , Maji Matitu (A) Mbagala Jijini Dar es Salaam akiwa nyumbani anapoishi huku akiwa na nyuso wa huzuni kufuatia changamoto ya maradhi yanayo msibu.

...........................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

Mzee Said Bakari Nyumbu (68) Mkazi wa Mtaa wa Ngurungu , Maji Matitu (A) Mbagala Jijini Dar es Salaam maisha yake yako hatarini kufuatia maradhi yanayomsibu na sasa anasubiri kufanyiwa upasuaji mwingine.

Mzee huyo ambaye hana ndugu anaishi kwa kusaidiwa na wasamaria wema baada ya bosi wake aliyekuwa akimsaidia kazi kushindwa kumsaidia kutokana na uzee.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Nyumbu anasema alizaliwa Kijiji cha Namikulo kilichopo Ruangwa Mkoa wa Lindi na kuwa ni mtoto wa pili katika familia yao ambayo imebaki na watoto wawili yeye na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Juma ambaye yupo kijijini kwao.

Alisema wazazi wake wote wawili walikwisha fariki pamoja na ndugu zake wawili aliowataja kuwa ni Abdul Bakari na Seleman Bakari.

Nyumbu anasema alisoma Shule ya Msingi Ndekenyela ambapo alihitimu mwaka 1971 na baada ya hapo alifika Dar es Salaam kwa baba yake mdogo Hassan Hamisi Ntimbwani aliyedai kuwa alikuwa derevs wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Anasema akiwa kwa baba yake huyo aliyekuwa akiishi Kinondoni alianza kufanya biashara ndogondogo  na baadae alipanga chumba ambapo alioa na kupata mtoto ambaye alifariki pamoja na mama yake.

Mzee Nyumbu anasema mwaka 2000 alifika Majimatitu mwenyeji wake akiwa ni Ester  Kachale ambaye alikuwa ni Muuguzi ambaye alikuwa akimsaidia kazu mbalimbali za nyumbani na ulinzi wa shamba lake.

Anasema mama huyo alikwisha staafu na sasa na amezeeka hana tena uwezo wa kunisaidia bali amenipa vyumba viwili vya kuishi.

Mzee Nyumbu anasema alikuwa akifanya kazi mbalimbali za vibarua kama za kubeba mchanga zilizokuwa zikimsaidia kupata fedha za kujikimu kimaisha lakini sasa hajui hatima ya maisha yake kutokana na maradhi yanayomsumbua.

Anasema changamoto aliyonayo ni usikivu hafifu, Tezidume na anakidonda katika moja ya vidole vyake ambacho kila siku kimekuwa kikiongezeka hivyo kumfanya akate tamaa ya kuishi.

Anasema alikwenda Hospitali ya Serikali ya Zakhiem ambapo aliambiwa kidole hicho kinatakiwa kukatwa kwa gharama ya Sh. 150,000 na kufanyiwa upasuaji wa tezidume kwa gharama ya  Sh. 700,000 pesa ambayo hana.

“Hivi sasa naishi kwa kusaidiwa na majirani zangu ambao nikizidiwa wanachangishana na kunipeleka hospitali nikipata matibabu natamani nirudi kijijini kwa mdogo wangu Juma lakini ndiyo hivyo sielewi hatima ya maisha yangu nawaombe watanzania wenzangu mnisaidie ndugu yenu nipate fedha za matibabu,” alisema Mzee Nyumbu huku akionekana kukata tamaa ya maisha.

Ndugu watanzania hayo ndiyo madhira anayopitia Mzee wetu huyu anaomba msaada wa hali na mali ili aweze kupata fedha za kumsaidia kupata matibabu yake na fedha za kujikimu kimaisha.

Kama utaguswa kumsaidia unaweza kuwasiliana na Mzee Ally Abdallah Ngurungu na Mjumbe wa Shina namba Nne Mwajuma Mshana ambao wanamsaidia kwa namba ya simu 0784679755 au Mwandishi wa Taarifa hii kwa namba ya simu 0754362990 kwa maelezo zaidi. Kutoa ni moyo na Mungu atakubariki kwa utoaji wako.

Shime watanzania kwa umoja wetu tushirikiane iwe kwa fedha na mawazo kuokoa maisha ya mzee wetu huyu.

Wakati tukiingia hewani taarifa tulizopata ni kwamba mzee huyo tayari amekwisha katwa kidole hicho lakini kutokana na kuathirika zaidi anatakiwa akatwe tena sehemu ya juu ya mguu wake huo.

Changamoto ya Mzee huyu imeibuliwa na Wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Matitu A,  ikiwa ni moja ya njia ya kutatua changamoto za wananchi. Wajumbe hao ni Hawa Omari na Jihadi Umwagala.

Mzee Nyumbu akiwa katika mawazo kufuatia maradhi yanayo msumbua.
Mzee Nyumbu akiwa na Mzee Ally Abdallah Ngurungu ambaye amekuwa akimsaidia kwa kushirikiana na wasamaria wema.
Mzee Nyumbu akiwa na Mzee Ally Abdallah Ngurungu. 

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad