TUNAPOCHANGIA MABILIONI TUMCHANGIE PIA MZEE HUYU - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, August 14, 2025

TUNAPOCHANGIA MABILIONI TUMCHANGIE PIA MZEE HUYU

Ana miaka 68, amekwisha katwa kidole, anasubiri kukatwa mguu

Anachangamoto ya kutosikia, anasaka 700,000 afanyiwe upasuaji wa tezi dume

Yupo Temeke Hospitali akipigania uhai wake, anasaidiwa na wasamaria wema

Mzee Said Bakari Nyumbu (68) Mkazi wa Mtaa wa Ngurungu , Maji Matitu (A) Mbagala Jijini Dar es Salaam, akiwa katika nyumba anayoishi.

.......................................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKATI Watanzania wenye mapenzi mema na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekichangia chama hicho zaidi ya Sh. Bilioni 86,  Mtanzania mwenzetu na mpiga kura Mzee Said Bakari Nyumbu (68) Mkazi wa Mtaa wa Ngurungu , Maji Matitu (A) Mbagala Jijini Dar es Salaam maisha yake yako hatarini kufuatia maradhi  yanayomsibu yanayohitaji msaada,

Mzee huyo sasa  amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Wodi namba saba (7) ya Wanaume akisubiri  kufanyiwa upasuaji wa pili wa kukatwa mguu baada ya awali kukatwa kidole chanzo chake kikiwa kujichoma na kitu chenye makali.

Ni jambo zuri na jema kwa watanzania kuwa na mapenzi ya kushiriki shughuli za kisiasa hasa katika chama wanachokipenda cha CCM ikiwemo kukichangia lakini tusiegemee tu kwenye siasa bali tuangalie pia maeneo mengine ya kijamii kwa kusaidia wananchi wenye changamoto mbalimbali.

Mzee huyo anachangamoto ya kutosia, amekatwa kidole cha mguuni lakini kutokana na kuathirika zaidi mguu wake unatakiwa ukatwe na hivi ninapoandika taarifa hii yupo Temeke Hospitali akisubiri kukatwa mguu huo.

Mbali ya kukatwa mguu pia anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa tezi dume lakini ameshindwa kufanyiwa baada ya kukosa Sh. 700,000 kama alivyoambiwa na daktari na hivyo kuendelea kuishi kwa mateso na maumivu makali.

Mzee huyo ambaye hana ndugu anaishi kwa kusaidiwa na wasamaria wema baada ya bosi wake aliyekuwa akimsaidia kazi kushindwa kufanya hivyo kutokana na uzee baada ya kustaafu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Nyumbu anasema alizaliwa Kijiji cha Namikulo kilichopo Ruangwa Mkoa wa Lindi na kuwa ni mtoto wa pili katika familia yao ya watoto wanne ambayo sasa imebaki na watoto wawili, yeye na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Juma ambaye yupo kijijini kwao.

Anasema wazazi wake wote wawili walikwisha fariki pamoja na ndugu zake hao wawili aliowataja kuwa ni Abdul Bakari na Seleman Bakari.

Hata hivyo Nyumbu anasema alisoma Shule ya Msingi Ndekenyela ambapo alihitimu mwaka 1971 na baada ya hapo alifika Dar es Salaam kwa baba yake mdogo Hassan Hamisi Ntimbwani aliyedai kuwa alikuwa dereva wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Anasema akiwa kwa baba yake huyo aliyekuwa akiishi Kinondoni alianza kufanya biashara ndogondogo  na baadae alipanga chumba ambapo alioa na kupata mtoto ambaye alifariki pamoja na mama yake.

Aidha, Mzee Nyumbu anasema mwaka 2000 alifika Majimatitu mwenyeji wake akiwa ni Ester  Kachale aliyekuwa Muuguzi Hospitali ya Serikali ya Mbagala Zakhem aliyekuwa akimsaidia kazi mbalimbali za nyumbani na ulinzi wa shamba lake.

Anasema mama huyo alikwisha staafu na sasa amezeeka hivyo hana tena uwezo wa kumsaidia bali amemuachia vyumba viwili vya kuishi.

Mzee huyo ameongeza kuwa alikuwa akifanya kazi mbalimbali za vibarua kama za kubeba mchanga zilizokuwa zikimsaidia kupata fedha za kujikimu kimaisha lakini sasa hajui hatima ya maisha yake kutokana na maradhi yanayomsumbua.

Ameongeza kuwa  changamoto aliyonayo ni usikivu hafifu, Tezidume na kidonda katika moja ya vikidole vyake ambacho kila siku  kimekuwa kikiongezeka hivyo kumfanya akate tamaa ya kuishi.

Anasema alikwenda Hospitali ya Serikali ya Zakhiem ambapo aliambiwa kidole hicho kinatakiwa kukatwa kwa gharama ya Sh. 150,000 na pia afanyiwe upasuaji wa tezidume kwa Sh. 700,000 pesa ambayo hana.

“Hivi sasa naishi kwa kusaidiwa na majirani zangu ambao nikizidiwa wanachangishana na kunipeleka hospitali.

Nikipata matibabu natamani nirudi kijijini kwa mdogo wangu Juma lakini ndiyo hivyo sielewi hatima ya maisha yangu, nawaomba watanzania wenzangu mnisaidie ndugu yenu nipate fedha za matibabu,” alisema Mzee Nyumbu huku akionekana kukata tamaa ya maisha.

Ndugu watanzania hizo ndiyo shida anazopitia mzee wetu huyu, anaomba msaada wa hali na mali ili aweze kupata fedha za kumsaidia kupata matibabu na fedha za kujikimu.

Kama utaguswa kumsaidia unaweza kuwasiliana na Mzee Ally Abdallah Ngurungu na pia  Mjumbe wa Shina namba Nne Mwajuma Mshana ambao wanamsaidia kwa namba ya simu 0784679755 (Ally Abdallah Ngurungu) au Mwandishi wa Taarifa hii kwa namba 0754362990 kwa maelezo zaidi. Kutoa ni moyo na Mungu atakubariki kwa utoaji wako.

Shime watanzania kwa umoja wetu tushikamane kama tulivyofanya kwa kuchangia chama chetu pendwa cha CCM kumsaidia mzee wetu Saidi Nyumbu kuokoa maisha yake

Mapema wiki hii (Agosti 12, 2025),  Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua harambee kwa ajili ya kuchangisha fedha za kampeni za chama hicho, wananchi, wana CCM na wapenzi wa chama hicho walionesha mapenzi ya dhati kwa kujitokeza kwa wingi kuchangia harambee hiyo iliyozinduliwa Ukumbi wa Mlimani City , ambapo takribani Sh. Bilioni 86 zilipatikana huku zoezi hilo likiendelea.

Changamoto ya ugonjwa ya Mzee Saidi Nyumbu imeibuliwa na Wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Matitu A kupitia CCM, ikiwa ni moja ya njia ya kutatua changamoto za wananchi wajumbe hao ni Hawa Omari na Jihadi Umwagala. 

Mzee Said Bakari Nyumbu (68) Mkazi wa Mtaa wa Ngurungu , Maji Matitu (A) Mbagala Jijini Dar es Salaam, akiwa na Mzee Ally Abdallah Ngurungu anayemsaidia. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad