LAZARO NYALANDU ASAKA KURA ZA WAGOMBEA CCM - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, September 12, 2025

LAZARO NYALANDU ASAKA KURA ZA WAGOMBEA CCM

Kada wa CCM, Lazaro Nyalandu
........................................ 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinaendelea na kampeni za uchaguzi nchi nzima baada ya kuzinduliwa rasmi Agosti 28, 2025 Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ambaye anagombea nafasi ya urais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

CCM ilianza kampeni hizo baada ya kuhitimisha mchakato wa uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na urais ambapo wanachama wengi walijitokeza kuomba ridhaa ya kuomba kuteuliwa na kupigiwa kura za maoni. 

Katika kura hizo za maoni wengi waliomba wakiwemo madiwani na  wabunge waliokuwa wakitumikia nafasi hizo kwenye majimbo mbalimbali hawakubahatika kurudi baada kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), kuteua wagombea ambao wameingia katika kampeni za chama hicho ili kuchuana na wagombea wa vyama vingine kwa lengo la kushika dola. 

Hata hivyo, kuchaguliwa na kutochaguliwa ni demokrasia iliyojengeka ndani ya chama hicho ikiwemo utaratibu wa kupokezana kijiti cha uongozi kwa wanachama wa chama hicho. 

Kwa wale wanachama waliopitishwa kugombea nafasi hizo kwao ni furaha lakini kwa wale ambao hawakuchaguliwa na kupitishwa kwao imekuwa ni maumivu makubwa ambao baadhi yao wameshindwa hata kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa uchaguzi na kuungana na walioteuliwa katika kampeni ambazo zimepamba moto nchini kote. 

Kutoungana na wenzao hao ili kuhakikisha chama chao kinapata ushindi ni kutokomaa kisiasa kwani jambo linaloangaliwa hapo ni chama na siyo mtu hivyo wanapaswa kushiriki katika kampeni hizo badala ya kuzisusia. 

Tumeona baadhi ya makada wa chama hicho ambao hawakuchaguliwa na wengine wao walikuwa ni mawaziri wakionesha ukomavu wao wa kisiasa wakiingia kwenye kampeni kutafuta kura za wagombea walioteuliwa jambo ambalo ni zuri. 

Mkoani Singida katika Jimbo jipya la Ilongero mmoja kati ya wana CCM aliyeomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge lakini hakupata nafasi hiyo ni Lazaro Nyalandu ambaye ni Waziri Mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. 

Mbali ya kukosa nafasi hiyo hajarudi nyuma bali amechochea moto wa kuhakikisha anaungana na wagombea wote wanaogombea nafasi za udiwani, ubunge na urais kutafuta kura za kutosha ili chama hicho kishike dola. 

Nyalandu ni kiongozi mwenye hulka ya upole na upendo,  wakati wote amekuwa akijitoa kusaidia chama hicho  kwa kutoa michango mbalimbali bila ya kinyongo na hiyo inatokana na kukipenda chama hicho ambacho ni kikongwe si kwa Tanzania tu bali na  Bara la Afrika kwa ujumla.

Nyalandu akizungumza Septemba 2, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za CCM Mkoa wa Singida, alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atahakikisha anapiga kampeni nzito ambazo zitaufanya mkoa huo kuongoza Tanzania kwa kura nyingi za CCM.

Amesema kwa hali na mali atawanadi mgombea urais kupitia CCM Dk.Samia Suluhu Hassan, wagombea udiwani na ubunge ndani ya Mkoa wa Singida na maeneo mengine ya nchi.

 “CCM ni chama ambacho kimetutoa mbali, ni chama kikubwa kuliko mgombea mmoja mmoja, tunataka tarehe 29, Oktoba kura za CCM Singida ziongoze Tanzania,mikoa itashindana tunataka ahadi yetu ya kumpa mama Dk.Samia Suluhu Hassan ziongoze, tunataka kura za madiwani na wabunge zikiongoze kuanzia wagombea wote wa mkoa wetu wa Singida nan chi kwa ujumla,” alisema Nyalandu huku akishangiliwa.

Nyalandu alimtaka kila mtu mwenye kadi ya kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025 atoke akapige kura na kuwachagua wagombea wote wanaotokana na CCM kuanzia diwani, mbunge na rais.

Alisema katika kipindi hiki cha liwe jua iwe baridi watapita nyumba kwa nyumba, tawi kwa tawi, kata kwa kata,jimbo kwa jimbo na kuwa watafanya kampeni hiyo nchi nzima yaani mikoa yote kwa kutumia basi kubwa la Mama Samia ambalo tayari limekwisha anza kazi rasmi.

Makala hii imeandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754362990)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad