MPO WAPI WATIA NIA, MBONA HATUWAONI KWENYE KAMPENI? - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, September 13, 2025

MPO WAPI WATIA NIA, MBONA HATUWAONI KWENYE KAMPENI?

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono  wananchi wa Wilaya ya Uyui katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Tabora  Septemba 11, 2025.

Wananchi wa Wilaya ya Uyui wakiwa kwenye mkutano huo wa kampeni.

................................

Na Dotto Mwaibale 

Kasi ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambapo watanzania watapiga kura kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani, na upande wa Zanzibar pia kumchagua Rais na Wawakilishi, inazidi kushika kasi.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kampeni hizo zilifunguliwa rasmi Agosti 28, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam na mgombea urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na maelfu ya wana-CCM na wananchi waliomiminika kushuhudia mwanzo wa safari ya kisiasa kuelekea sanduku la kura.

Kabla ya hatua ya kampeni, CCM ilikamilisha mchakato wa uteuzi wa wagombea wake. Hapo ndipo tulipoona wingi wa wanachama waliojipima kuwania nafasi mbalimbali. 

Kwa mujibu wa aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, watia nia wa ubunge peke yake walikuwa 3,585 kutoka Tanzania Bara, huku Zanzibar ikileta watia nia 524. 

Aidha, kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walijitokeza wagombea 503, na kwa ujumla wagombea wote ngazi zote, wakiwemo madiwani, walifikia zaidi ya 20,000.

Hii ni rekodi kubwa katika historia ya uchaguzi ndani ya CCM tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, jambo linaloonyesha mwamko wa wanachama kushiriki katika siasa na uongozi.

Hata hivyo, pamoja na hamasa kubwa ya watia nia wakati wa kuchukua fomu, hali imekuwa tofauti baada ya uteuzi kukamilika.

 Ni wachache tu walioungana kwa dhati na wagombea walioteuliwa ili kushiriki kikamilifu kwenye kampeni za chama.

Swali linalojitokeza ni: Mpo wapi watia nia? Mbona hatuwaoni kwenye kampeni?

Inaonekana baadhi yao wamesalia kimya, huenda kwa sababu ya kukosa uteuzi, na wengine wakiamua “kukaa pembeni” kana kwamba jukumu lao liliishia kwenye kuchukua fomu pekee.

Ni ukweli kwamba si kila aliyeomba ridhaa ya chama anaweza kuteuliwa, kwa kuwa nafasi ni chache ikilinganishwa na idadi ya waombaji. 

Lakini, dhamira ya kweli ya “ufia chama” inadhihirika si wakati wa kuchukua fomu pekee, bali hasa katika kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha ushindi wa chama chenyewe.

Kura haziwezi kupatikana bila kampeni. Kura haziwezi kujikusanya zenyewe bila mshikamano wa wanachama wote—wale walioteuliwa na wale ambao hawakuteuliwa.

 Ndio maana CCM na vyama vingine huendesha kampeni ili kuhamasisha wananchi, kunadi sera na ilani, na kuvuna kura za ushindi.

Tayari tumeona baadhi ya watia nia waliokosa uteuzi wakijitokeza hadharani, wakiahidi kushirikiana usiku na mchana kuhakikisha wagombea wa chama chao wanashinda.

Hawa ndiyo wanaodhihirisha uadilifu wa kweli wa kisiasa, kwani kwao chama kipo juu ya maslahi binafsi.

Lakini, bado pengo linaonekana. Ni wangapi kati ya wale maelfu ya watia nia wako mstari wa mbele kwenye mikutano ya kampeni, mikutano ya hadhara, na vikao vya uhamasishaji vijijini na mitaani?

Leo, CCM ipo katika hatua ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu. Ni dhahiri kwamba mafanikio yake yanategemea mshikamano wa kila mwana-CCM, si viongozi pekee. 

Ndiyo maana tunalazimika kuuliza kwa sauti ya juu, "mpo wapi watia nia? Mbona hatuwaoni kwenye kampeni?”

Kwa hakika, historia haitawakumbuka kwa kuchukua fomu pekee, bali kwa nafasi yenu ya kushirikiana kulinda na kuimarisha chama chenu wakati kinapohitaji mshikamano zaidi.

Wananchi na Wana CCM wa Wilaya ya Uyui wakiwa kwenye mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad