USHIROMBO YANG’ARA: MWENGE WA UHURU WAKAGUA MRADI WA BARABARA YA LAMI NYEPESI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, September 5, 2025

USHIROMBO YANG’ARA: MWENGE WA UHURU WAKAGUA MRADI WA BARABARA YA LAMI NYEPESI

Mkuu wa Wilaya ya Bukonbe, Pskas Muragili aliyeshika kipaza sauti akimuomba mkimbiza Mwenge kitaifa kukagua mradi huo.

...................................

Mji wa Ushirombo, Wilaya ya Bukombe, umeendelea kunufaika na miradi ya maendeleo baada ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, ukiongozwa na Ndugu Ismail Ali Ussi, kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami nyepes (double surface dressing) yenye urefu wa kilomita 3.25.

Mradi huu, unaotekelezwa kwenye kata za Igulwa na Katente, ulianza Septemba 27, 2024 na unatarajiwa kukamilika Septemba 15, 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.57, fedha kutoka serikali kuu kupitia tozo ya mafuta. Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 43, ambapo kazi zilizokamilika ni uchimbaji wa udongo usiofaa na ujenzi wa tabaka tatu za udongo (Fill, G15 na G45). Kazi inayoendelea ni ujenzi wa makalvati, huku zilizobaki zikiwa ni ujenzi wa tabaka kuu, mifereji, uwekaji wa lami, taa na alama za barabara.

Baada ya kukagua, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru ametoa pongezi kwa TARURA kwa kusimamia mradi kwa viwango bora na kuwataka wahakikishe ubora huo unaendelea hadi kukamilika. Aidha, amewataka wananchi kuulinda mradi huo kwa kutotupa taka kwenye mitaro na kuutunza kama mali ya jamii.

Akizungumza kwa niaba ya TARURA, Meneja wa Bukombe, Eng. E. Msumba Msoka, alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa wakazi wa Ushirombo, ikiwemo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza changamoto za mafuriko na kurahisisha biashara usiku na mchana kutokana na taa za barabarani zitakazofungwa.

Miongoni mwa wananchi waliofurahishwa na mradi huo ni Anna James, mfanyabiashara wa mgahawa, ambaye alisema: “Kama unavyoona magari yakipita vumbi ni jingi na linatuathiri, lakini mradi huu ukikamilika hakutakuwa na vumbi tena. Pia taa zitakazowekwa zitafanya biashara zetu ziendelee hata usiku.”

Wananchi wamepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huu unaobeba ahadi ya kuboresha maisha yao. Viongozi wa Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, nao wametajwa kwa utekelezaji makini wa maagizo yaliyotolewa katika maandalizi ya mradi huo.

Mradi huu, licha ya kuwa haujakamilika, umeelezwa kuwa ni mfano bora wa namna serikali inavyotekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi na viwango vya juu, ukiakisi dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi mijini na vijijini bila kuchoka.

Wakimbiza mwenge kitaifa wakifanya ukaguzi  wa mradi kabla ya kuupitisha
Wakimbiza Mwenge kitaifa wakifuatilia kwa makini wakati mainjinia wakikagua mradi  huo
Mkimbiza Mwenge kitaifa akipokea maelezo ya mradi kutoka timu ya ukaguzi.
Mkimbiza Mwenge kitaifa akipokea maelezo ya mradi kutoka kwa Meneja w Tarura Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msumba
Ukaguzi wa miradi ukiendelea.
Burudani zikitolewa 


   Imeandaliwa na Victor Bariety 0757 856 284

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad