Meneja wa Sokoni Micro Finance, Kelvin Joseph, akikabidhi msaada wa futari kwa Wazee wa Zingiziwa Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.
.................................................
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Sokoni Micro Finance imetoa msaada wa futari kwa Kikundi cha Wazee wanaoishi Kata ya Zingiziwa, Ilala jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Sokoni Micro Finance, Kelvin Joseph, alikabidhi msaada huo wa futari ikiwamo sukari na tambi kwa niaba ya mkurugenzi wa kampuni hiyo, Kahlan Mazrui. Kikundi hicho kinachojulikana Wazee Amani Group Tanzania, kilianzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kutatua changamoto zao.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, mwenyekiti wa kikundi hicho, Msahilo Mbegu aliupongeza uongozi wa Sokoni Micro Finance kwa kuwakumbuka katika kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani."Niishukuru kampuni ya sokoni microfinance, ilikuwa na moyo mkubwa wa kutusaidia mashine ya kufyatulia matofari, lakini wamekwama mahali, lakini tunashukuru msaada tuliopata," alisema Mbegu.
Alisema kikundi chao kilianzishwa baada ya mwenzao kuishi mazingira magumu yaliyomsababishia kuishi kwa kula udogo na baadaye kufariki kutokana na kukosa matunzo. Mbegu alisema tangu wameanzisha kikundi chao hawapati msaada wowote kutoka serikalini huku hali zao maisha zikiwa duni.
Pia Mbegu alisema kutokana na kukosa nafasi uwakilishi katika vyombo vya maamuzi, kama baraza la kata, madiwani na mbunge ni moja ya tatizo, kwa kuwa hakuna wa kuwasemea changamoto zao. Pamoja na kwamba wana madiwani na wabunge, lakini hawakumbuki kama kuna Wazee ambao wanatakiwa kupewa msaada na serikali yao.
"Tunashindwa kusaidiwa hata panado, serikali imetuacha hatuna msaada wowote katika kikundi chetu," alisema. Mbegu aliiomba serikali, taasisi za umma, kampuni mbalimbali binafsi kuwatupia jicho la tatu kama walivyofanya Sokoni Micro Finance.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Sokoni, Mazrui baada ya kukabidhi msaada huo, meneja wa kampuni hiyo, Joseph alisema imekuwa ni kawaida kwao kurudisha faida kwa jamii yenye uhitaji. Joseph alisema pamoja na kukabidhi msaada huo, lakini atafikisha changamoto cha Wazee hao kwa mkurugenzi wao ili aone jinsi ya kuwasaidia zaidi.
"Tumesikia ni udhuni mkubwa mnashindwa kupata hata panado tutakuja kuwasikiliza kutokana na changamoto zenu," alisema Joseph.
Naye mmoja wa Wazee wa kikundi hicho, Lukia Mohamed aliishukuru Kampuni ya Sokoni Micro Finance kwa kuwapatia futari.










No comments:
Post a Comment