WAMACHINGA WAOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA SOKO LA BWERA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, March 7, 2026

WAMACHINGA WAOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA SOKO LA BWERA

 Meneja wa Soko la Bwera, Julius Faustine, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani kuhusu uwekezaji huo.

.................................. 

 Na Mwandishi Wetu.

WAFANYABIASHARA wadogo wadogo maarufu wamachinga, wameombwa kuchangamkia sehemu za kufanyia kazi katika Soko la Bwera, lililopo Kata ya Majohe, Ilala, jijini Dar es Salaam.

 Ombi hilo lilitolewa na meneja wa soko hilo, Julius Faustine, wakati akizungumzia uwekezaji wa miundo mbinu bora iliyofanyika katika soko la Bwera  kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.          

Faustine alisema soko hilo ambao ni jipya linachukua zaidi ya wafanyabiashara 200 huku akiwaomba kuwahi nafasi zilizopo ili waweze kufanya biashara kwa utulivu bila usumbufu.

Meneja huyo alisema soko hilo limeanzishwa ili kuwapunguzia wananchi wa Majohe kufuata mahitaji umbali mrefu, kwani mahitaji yote yanapatikana katika soko la Bwera kwa bei nafuu.

 "Tunawakaribisha sana wamachinga ambao hawana sehemu ya kufanya biashara waje Bwera, nafasi zipo kwa ajili ya biashara mbalimbali," alisema Faustine. 

Alisema soko hilo, linafikika kirahisi kwa usafiri wa magari makubwa na madogo, licha ya kuwapo kwa changamoto ndogo ndogo za miundo mbinu.

Naye, Amina Mtupa ambaye ni mjasiliamali katika soko hilo, aliupongeza uongozi wa Bwera kwa kuweka mazingira bora ya kufanya biashara zao.

Amina alisema soko hilo lina umuhimu mkubwa kwa wakazi wa Majohe, kwani limewapunguzia umbali mrefu wa kufuata mahitaji ya kila siku.

Mwanamama mjasiliamali huyo, alisema kutokana na miundo mbinu ya soka hilo kuwa bora, kunawawezesha kufanya biashara bila usumbufu, lakini bei ya bidhaa ikiwa ya chini ukilinganisha na masoko mengine.

Kwa upande wake, William Godfrey, ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanafanya shughuli zao pembezoni mwa barabara kwenda soko la Bwera ili waweze kupata eneo la kufanya biashara zao.

Godfrey alisema kabla ya kuhamishia biashara yake katika soko hilo, walikuwa wanafanya shughuli zake Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana na ubora wa soko la Bwera mfanyabiashara yeyote anaweza kubuni biashara yake na ikaenda vizuri, kwani mahitaji yamekuwa ni makubwa kwa wakazi wa maeneo ya Majohe, Kivule na mengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad