Ziara ya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba mjini Iringa Jumamosi Mei 23, 2026 iligeuka kuwa jukwaa zito la wananchi kufikisha kilio chao moja kwa moja serikalini, baada ya mkazi mmoja kusimulia kwa uchungu namna gari lake lilivyoteketea kwa moto likiwa mikononi mwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika mkutano wa hadhara uliokuwa ukisikiliza kero za wananchi, Odilo Boniface Ngamilaga alisimama mbele ya Waziri Mkuu na kueleza simulizi iliyoacha mamia ya wananchi wakiwa kimya kwa mshangao, huku wengine wakionyesha hisia za masikitiko na hasira.
Ngamilaga alisema alinunua gari lake kwa njia halali na kulifikisha Iringa bila kujua kuwa watu waliomuuzia walikuwa hawajakamilisha taratibu za ushuru. Alisema baadaye maofisa wa TRA walifika katika duka lake na kulichukua gari hilo kwa ajili ya uchunguzi.
Alieleza kuwa alipofikishwa katika ofisi za TRA kutoa maelezo, aliwaambia maofisa hao kwamba wauzaji walimuahidi kumpatia nyaraka nyingine zote baadaye huku yeye akiwa amekabidhiwa risiti pekee wakati wa manunuzi.
Kwa mujibu wa mlalamikaji huyo, baada ya maelezo yake TRA ilimtaka kulipa shilingi milioni 4 na elfu 26 ili aweze kurejeshewa gari lake. Alisema aliiomba mamlaka hiyo impatie nafasi ya kulipa kwanza sehemu ya fedha hizo huku akimalizia kiasi kilichobaki baadaye, lakini ombi lake lilikataliwa.
Ngamilaga alisema alikubali masharti hayo na akaendelea kutafuta fedha hadi alipokamilisha kiasi alichoelekezwa. Hata hivyo, aliporejea TRA kwa ajili ya kulipa na kuchukua gari lake, alidai alipokelewa kwa maneno ya pole yaliyomchanganya.
“Nilipouliza mnanipa pole ya nini ndipo wakaambia gari yako imeungua,” alieleza mbele ya Waziri Mkuu huku akidai gari hilo hadi sasa bado limo katika eneo la TRA Iringa likiwa limeteketea kwa moto.
Kauli hiyo ilimfanya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba kuingilia kati na kumtaka Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Peter Jackson, kutoa maelezo kuhusu tukio hilo lilivyotokea wakati gari hiyo ikiwa chini ya mamlaka yao.
“Mmechukua gari, mmeikaa nayo, mmeunguza moto, kwanini mmeishia kutoa pole?” alihoji Waziri Mkuu mbele ya wananchi waliofurika katika mkutano huo.
Katika majibu yake, Meneja wa TRA Iringa Peter Jackson alisema angependa kukaa na wasaidizi wa Waziri Mkuu ili kutoa maelezo ya kina kuhusu suala hilo, kauli iliyozua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Baada ya kusikiliza maelezo yote, Waziri Mkuu alitoa agizo kwa TRA kufanya tathmini ya thamani ya gari hilo na kuhakikisha mmiliki wake anafidiwa.
Hata hivyo, siku iliyofuata, TRA kupitia taarifa ya Idara ya Elimu na Mawasiliano kwa Umma Mkoa wa Iringa ilisema itaendelea kumsikiliza mlalamikaji huyo ili kupata ufumbuzi kwa mujibu wa sheria na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.










No comments:
Post a Comment