Dk. Mwigulu
ametoa pongezi hizo Juni 27, 2026) alipokuwa akiweka jiwe la msingi la Jengo la
Taaluma la TIA, Kampasi ya Singida
wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida.
“Jengo hili la chuo chetu lipo Singida ni hatua kubwa sana. Hongereni bodi, hongereni chuo, hongereni wanafunzi, Tunawatakia kila la heri," alisema Dk. Mwigulu.
Mwigulu
alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ya juu kwa kuboresha miundombinu
ya kujifunzia na kufundishia ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo
wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Alisema ujenzi wa jengo hilo ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha mazingira ya elimu ya juu na kusogeza huduma hizo kwa wananchi.
Dk. Mwigulu
alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wahandisi, washauri na wakandarasi wazawa
wanaotekeleza mradi huo na kueleza kuwa ushiriki wao unaonesha uwezo mkubwa katika
kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
Waziri Mkuu
Dk. Mwigulu aliongeza kuwa amefurahishwa kuona wahandisi wanaojenga mradi huo ni
wazawa na Rais Samia alielekeza lazima tujenge uchumi unaomilikiwa na
Watanzania na kujenga sekta binafsi ya ndani sambamba na uwekezaji kutoka nje.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde, alisema Serikali imeendelea
kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuwekeza katika vyuo vya elimu ya juu ili
kuongeza upatikanaji wa elimu bora, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia,
kuimarisha tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia pamoja na kuzalisha
wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya
Taifa.
Alisema Wizara
ya Fedha itaendelea kuhakikisha rasilimali za Serikali zinaelekezwa katika
miradi yenye tija kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Taasisi ya
Uhasibu Tanzania (TIA).
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa. William Pallangyo akitoa taarifa ya ujenzi huo.
......................................
Akizungumza
katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA),
Profesa. William Pallangyo, alisema jengo hilo la taaluma lina ukubwa wa mita
za mraba 9,250 na litakuwa na kumbi za mafunzo, madarasa, kumbi za mihadhara,
ukumbi wa mikutano pamoja na ofisi za watumishi.
Alisema kumbi za mafunzo zitakuwa mbili zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 325 ukumbi wa kwanza ukiingiza wanafunzi 175 na wa pili 150.
Aidha, Pallangyo alisema kuwa katika jengo hilo kutakuwa na madarasa 9 kati ya madarasa hayo manane yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 250 na darasa moja wanafunzi 300 kwa wakati mmoja.
"Katika jengo hilo kutakuwa na kumbi za mihadhara mbili na kila ukumbi mmoja utakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 450 na kufanya jumla ya wanafunzi 900 kwa wakati mmoja," alisema.
Akizungumzia ofisi alisema ni 15 na zitakuwa na uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa kila moja hivyo kuwa na watumishi 30 kwa wakati mmoja na pia kutakuwa na ukumbi mmoja wa mikutano ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 25.
Alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 13.5 umefikia asilimia 63 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2026.
Aidha, Pallangyo ameiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa mabweni ili kukidhi ongezeko la wanafunzi litakalotokana na kukamilika kwa mradi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Prof. Jehovaness Aikaeli, amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati, huku akieleza kuwa mradi huo utachangia kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi kwa maendeleo ya Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Prof. Jehovaness Aikaeli.
.........................................
Mhandisi Mkazi Mshauri wa Mradi huo, Henry Chundu, akizungumza kwenye hafla hiyo alisema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi wapatao 3,500 kwa wakati mmoja na limejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa, ikiwemo mifumo ya usalama dhidi ya moto, matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Hafla hiyo ikiendelea.
Wageni waalikwa wakiwa kwenye hafla hiyo.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (kushoto) na Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallanyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la taaluma la Taaisisi ya Uhasibu Tanzania Kampasi ya Singida, Juni 27, 2026.
Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akipokea taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. Jehovaness Aikael, baada ya kuweka jiwe la Msingi Jengo la Taaluma, katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, lililokamilika kwa asilimia 63, katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya TIA, Prof. William Pallangyo.
Waziri Mkuu Dk.Mwigulu akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa TIA Kampasi ya Singida ambao ni wanufaika wa Mradi huo.















No comments:
Post a Comment