𝐖𝐀𝐍𝐀𝐅𝐔𝐍𝐙𝐈 𝟐𝟒𝟔,𝟏𝟗𝟕 𝐖𝐀𝐋𝐈𝐎𝐏𝐀𝐍𝐆𝐈𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐔𝐍𝐆𝐀 𝐊𝐈𝐃𝐀𝐓𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐎 𝐖𝐀𝐍𝐀𝐏𝐀𝐒𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐑𝐈𝐏𝐎𝐓𝐈 𝐒𝐇𝐔𝐋𝐄𝐍𝐈 𝐉𝐔𝐋𝐀𝐈 𝟎𝟒, 𝟐𝟎𝟐𝟔 - 𝐏𝐑𝐎𝐅. 𝐒𝐇𝐄𝐌𝐃𝐎𝐄 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, June 2, 2026

𝐖𝐀𝐍𝐀𝐅𝐔𝐍𝐙𝐈 𝟐𝟒𝟔,𝟏𝟗𝟕 𝐖𝐀𝐋𝐈𝐎𝐏𝐀𝐍𝐆𝐈𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐈𝐔𝐍𝐆𝐀 𝐊𝐈𝐃𝐀𝐓𝐎 𝐂𝐇𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐎 𝐖𝐀𝐍𝐀𝐏𝐀𝐒𝐖𝐀 𝐊𝐔𝐑𝐈𝐏𝐎𝐓𝐈 𝐒𝐇𝐔𝐋𝐄𝐍𝐈 𝐉𝐔𝐋𝐀𝐈 𝟎𝟒, 𝟐𝟎𝟐𝟔 - 𝐏𝐑𝐎𝐅. 𝐒𝐇𝐄𝐌𝐃𝐎𝐄

Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema jumla ya wanafunzi 246,197 wakiwemo wasichana 114,102 na wavulana 132,095 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2026 wanatakiwa kuripoti shuleni kuanzia Julai 04, 2026 hadi Julai 31, 2026 kwakuwa muhula wa kwanza wa masomo utaanza Julai 06, 2026. 

Prof. Shemdoe amesema hayo leo Juni 01, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Magogoni Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka 2026.

“Wanafunzi 172,114 sawa na asilimia 69.9 wakiwemo wasichana 85,987 na wavulana 86,127 wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule  za sekondari za Serikali 856 zikiwemo shule za bweni 825, kutwa 25 na kutwa na bweni sita (06),” amefafanua Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe amesema jumla ya wanafunzi 74,083 sawa na asilimia 30.1  wakiwemo wasichana 28,115 na wavulana 45,968 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya Ufundi.

“Wanafunzi 3,144 wakiwemo wasichana 1,170 na wavulana 1,974 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo 04 vya elimu ya ufundi, vyuo hivyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI),” ameeleza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amesisitiza kwamba, uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule; hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kutokana na ukosefu wa nafasi.  

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizotumika kujenga miundombinu bora ya shule za kidato cha tano na vyuo vya kati ambayo itatumika kuwahudumia wanafunzi 246,197 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi mwaka 2026.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad