Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James (kulia), akizungumza na viongozi mbalimbali wakati akithibitisha mkoa huo kuanza rasmi kwa mashindano ya ngazi ya shule za msingi (UMITASHUMTA) ambayo yalianza Juni 7, 2026, yakifuatiwa na mashindano ya shule za sekondari (UMISSETA), ambapo kwa ujumla michezo yote itahitimishwa tarehe 30 Juni 2026.
.................................
Na Godwin Myovela, Iringa
Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kujenga nidhamu na kuandaa vijana wenye uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa.
Hata hivyo, nyuma ya ushindi wa medali na mafanikio ya timu, kuna jambo muhimu linalopaswa kulindwa; uadilifu na maadili mema.
Washiriki wa UMISSETA wamehimizwa kuzingatia uaminifu, heshima na nidhamu wakati wote wa mashindano ili kuhakikisha ushindani unakuwa wa haki na unaoendana na malengo ya elimu.
Wito huo umetolewa Juni 19, 2026 na Dkt. Emmanuel Shindika, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, wakati akizungumza katika Baraza la UMISSETA lililofanyika Shule ya Sekondari Lugalo, Manispaa ya Iringa.
Dkt. Shindika amesema udanganyifu katika michezo haukubaliki kwa kuwa unaharibu misingi ya ushindani wa haki na kupunguza thamani ya michezo katika kujenga vipaji na tabia za vijana.
Amesema washiriki wanapaswa kuelewa kuwa michezo ni sehemu ya elimu, hivyo nidhamu, uaminifu na kuheshimu kanuni ni sehemu ya mafanikio ya mwanafunzi.
“Niwaombe vijana wetu kuwa waadilifu michezoni na kuepuka tabia zisizofaa wakitambua kuwa michezo ni sehemu ya taaluma,” amesema Dkt. Shindika.
Ameongeza kuwa michezo inapaswa kuwa darasa la kujenga uwajibikaji, ushirikiano na heshima kwa wapinzani, badala ya kuwa njia ya kutafuta ushindi kwa gharama yoyote.
Katika safari ya maendeleo ya michezo nchini, uadilifu ni msingi wa kujenga wanamichezo wenye uwezo, nidhamu na kujiamini katika majukwaa makubwa.
Viongozi wa timu, walimu na walezi wametakiwa kuhakikisha vijana wanapata malezi sahihi ndani na nje ya viwanja ili kulinda heshima ya shule na mikoa wanayoiwakilisha.
Hatua za kinidhamu dhidi ya watakaokiuka kanuni za mashindano ni muhimu ili kulinda hadhi ya UMISSETA na kuhakikisha haki inakuwa msingi wa kila ushindani.
Kwa washiriki wa mwaka huu, ujumbe ni mmoja; shindaneni kwa nguvu, onyesheni vipaji, lakini msisahau kulinda maadili na heshima ya michezo.
UMISSETA 2026 si jukwaa la kutafuta mabingwa pekee, bali ni shule ya maisha inayojenga viongozi wa kesho wenye nidhamu, uzalendo na uwajibikaji.










No comments:
Post a Comment