Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Bi. Amina Seif (katikati), akiwa na Wana Kikundi cha Vijana cha Maendeleo Bodaboda.
.......................
Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri mbalimbali nchini imekuwa fursa muhimu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hasa kupitia uanzishaji na upanuzi wa shughuli za ujasiriamali.
Hata hivyo, kupata mkopo ni hatua moja, lakini kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha fedha hizo kwa wakati ni jambo jingine muhimu linalohitaji nidhamu, uaminifu na uwajibikaji.
Umuhimu wa kurejesha mikopo hiyo ni mkubwa kwa mkopaji, vikundi vya wanufaika na jamii kwa ujumla, kwa kuwa marejesho huwezesha fedha hizo kuendelea kutumika kuwasaidia wananchi wengine kujikwamua kiuchumi.
1. MAREJESHO
YA MIKOPO YA ASILIMIA 10 NI CHACHU YA MAENDELEO
Kurejesha mikopo ya asilimia 10 kwa wakati kuna faida nyingi, zikiwemo kuwawezesha wananchi wengine kupata mikopo, kuendeleza mfuko wa mikopo wa halmashauri na kukuza biashara pamoja na shughuli za uzalishaji mali.
Fedha zinaporejeshwa, zinaweza kutumika tena kukopesha vikundi vingine vyenye nia na mipango ya kujiendeleza kiuchumi. Hatua hiyo husaidia kuimarisha mzunguko wa fedha na kuhakikisha mpango huo unaendelea kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Aidha, mikopo inayotumika vizuri inaweza kusaidia kuongeza kipato, kupanua biashara, kuimarisha ajira na kupunguza umaskini. Kwa upande wa wanufaika, kurejesha mikopo kwa wakati huwajengea nidhamu ya kifedha na kuwasaidia kupanga mapato na matumizi yao kwa uwajibikaji.
Marejesho pia huimarisha uaminifu kati ya Serikali na wananchi, huku yakisaidia kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa Bungeni, Serikali imeimarisha mfumo wa kidijitali wa WEZESHA kwa ajili ya kuomba, kusimamia na kufuatilia mikopo hiyo pamoja na marejesho yake.
2. KIKUNDI
CHA BODABODA CHA MJI WA MBINGA CHANG'ARA KWA KUREJESHA MKOPO WA SHILINGI MILIONI 12.7
Kikundi cha vijana cha Maendeleo Bodaboda kilichopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, kimekuwa mfano wa kuigwa baada ya kukamilisha marejesho ya mkopo wa Shilingi milioni 12.7.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Bi. Amina Seif, akimkabidhi cheti Mwenyekiti wa Kikundi cha vijana cha Maendeleo Bodaboda , Ndugu Kefasi Kamage.
..............
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Bi. Amina Seif, amewapongeza vijana hao kwa kuonyesha nidhamu na uaminifu katika kurejesha mkopo huo.
Mkopo huo umesaidia kikundi hicho kupiga hatua za maendeleo baada ya kufanikiwa kununua pikipiki nne zinazotumika katika shughuli za bodaboda na kuongeza mapato ya kikundi.
Akizungumza na vijana hao, Bi. Seif amesisitiza kuwa mfano huo unathibitisha kuwa mikopo ya halmashauri inaweza kuwa chachu ya maendeleo ikiwa itatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameahidi kuwa halmashauri itaendelea kuwezesha makundi ya vijana na wanawake wenye nia thabiti ya kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bi. Cecilia Mbata, amesema kikundi hicho kimeonyesha mfano mzuri kwa kurejesha fedha hizo bila shuruti.
Bi. Mbata amewahimiza vijana wengine kujitokeza na kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu zilizowekwa na kutumia fedha hizo kwa uaminifu.
Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho, Ndugu Kefasi Kamage, kwa niaba ya wanakikundi wenzake, ameishukuru halmashauri kwa kuwaamini na kuwapatia mkopo huo ambao umewasaidia kuendeleza shughuli zao za biashara ya bodaboda.
Kamage amewahimiza vijana wengine kuepuka kukopa kwa ajili ya matumizi yasiyo ya uzalishaji, badala yake watumie mikopo hiyo kuanzisha au kukuza biashara na shughuli nyingine za kiuchumi, huku wakihakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili wananchi wengine nao wanufaike.
3. MIKOPO YA
ASILIMIA 10 NI FURSA YA UWEZESHAJI INAYOHITAJI UWAWAJIBIKAJI
Mikopo ya asilimia 10 ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia makundi yanayostahili kupata fursa hiyo kwa mujibu wa taratibu husika.
Kwa mujibu wa mfumo uliotumika katika mpango huo, fedha hizo zilitengwa kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa uwiano wa asilimia nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
Mikopo hiyo isiyo na riba imekusudiwa kuwapatia wanufaika mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Hata hivyo, mafanikio ya mpango huo yanategemea si tu upatikanaji wa mikopo, bali pia matumizi sahihi ya fedha hizo na utayari wa wanufaika kurejesha mikopo kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.
Mfano uliotolewa na Kikundi cha Maendeleo Bodaboda cha Halmashauri ya Mji wa Mbinga unaonyesha umuhimu wa uwajibikaji katika kutumia fursa za uwezeshaji wananchi.
Wanufaika wengine wanahimizwa kuiga mfano huo kwa kutumia mikopo kwa malengo ya uzalishaji, kusimamia vizuri biashara zao na kurejesha fedha kwa wakati. Hatua hiyo itasaidia kuendeleza mzunguko wa mikopo na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata nafasi ya kujikwamua kiuchumi.
Muonekano wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.Makala hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.












No comments:
Post a Comment