
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi (DAS), Ndugu Rashid Rashid (katikati aliyekaa), akiwa na viongozi wengine walioshiriki Tamasha la ngoma za asili lililoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida,Kata ya Iyumbu wakati wa utoaji wa elimu kuhusu rushwa.
...............
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, imeandaa tamasha la ngoma za asili katika Kata ya Iyumbu kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuimarisha uadilifu katika jamii.
Akizungumza katika tamasha hilo lililokuwa na kaulimbiu isemayo “Ngoma Zetu, Uadilifu Wetu,” Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo, alisema rushwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa kuwa hudhoofisha utoaji wa huduma bora, husababisha matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi zao.
Alisema rushwa pia inaweza kuwanyima wananchi haki zao za msingi na kuathiri maisha yao ya kila siku, kuanzia katika huduma za afya na elimu hadi utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kibwengo alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi na hayapaswi kuachiwa TAKUKURU pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
Akizungumzia umuhimu wa tamasha hilo, alisema si tukio la burudani pekee, bali ni jukwaa la kuunganisha utajiri wa utamaduni wa Kitanzania na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutumia sanaa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya vitendo hivyo, kuhamasisha uwajibikaji na kujenga misingi imara ya uadilifu.
Alisema jamii ina utajiri mkubwa wa mila, desturi, nyimbo, ngoma na sanaa mbalimbali ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitumika kuelimisha, kuonya, kukemea maovu na kuimarisha mshikamano.
Aliongeza kuwa ngoma za asili zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya jamii, zikisaidia kufikisha ujumbe na kurithisha maarifa na maadili kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
“Ni kwa kutambua nafasi hiyo ndipo TAKUKURU imeona umuhimu wa kutumia utajiri wetu wa kitamaduni kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuimarisha uadilifu,” alisema Kibwengo.
Alisema wasanii wana uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa wananchi kupitia nyimbo, maigizo, mashairi na midundo ya ngoma za asili, hivyo akavitaka vikundi vya ngoma kutumia vipaji vyao kuhamasisha jamii kukataa rushwa.
Alivitaka vikundi hivyo kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uadilifu katika familia na jamii, wajibu wa kila mwananchi katika kukataa kutoa au kupokea rushwa, uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma na madhara ya kutumia rushwa kupata huduma au upendeleo usiostahili.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwalea watoto katika misingi ya uaminifu, haki na uwajibikaji ili kujenga jamii inayothamini maadili mema.
Kibwengo alisema uadilifu hauishii katika ofisi za Serikali pekee, bali unaanzia nyumbani, shuleni, katika biashara, shughuli za kijamii na maeneo ya kazi.
Alifafanua kuwa mzazi au mlezi mwadilifu humfundisha mtoto kusema ukweli, mwalimu mwadilifu hutenda haki kwa wanafunzi wake, kiongozi mwadilifu hutanguliza maslahi ya wananchi, mfanyabiashara mwadilifu hufuata taratibu halali na mwananchi mwadilifu hukataa kutoa rushwa ili kupata huduma anayostahili.
“Hivyo basi, uadilifu ni wajibu wa kila mmoja wetu na si wa TAKUKURU pekee,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kukataa kutoa au kupokea rushwa ili kupata upendeleo usiostahili, kutoa taarifa za kweli zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tuhuma za rushwa na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Alisema ushiriki wa wananchi katika kufuatilia miradi ya maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
“Mapambano dhidi ya rushwa yanaanza na maamuzi yetu ya kila siku. Tunapokataa kutoa rushwa, tunalinda haki zetu. Tunapokataa kupokea rushwa, tunalinda dhamana tuliyopewa. Tunapotoa taarifa za vitendo vya rushwa, tunasaidia kuimarisha uwajibikaji,” alisema.
Kibwengo alitoa wito kwa wananchi wa Kata ya Iyumbu na Wilaya ya Ikungi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na TAKUKURU pamoja na viongozi wengine katika kujenga jamii inayokataa rushwa na kuthamini uadilifu.
Pia, aliwashukuru viongozi, watendaji wa Serikali, vikundi vya ngoma za asili na wananchi walioshiriki katika tamasha hilo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kuelimisha jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.
Alimalizia
hotuba yake kwa kusisitiza kaulimbiu isemayo: “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na
Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi, akizungumza.
Viongozi meza kuu wakiwa na mmoja wa wasanii katika tamasha hilo.
Burudani zikiendelea
Wananchi wakiwa Kata ya Iyumbu kwenye tamasha hilo
Viongozi wakiwakwenye tamasha hilo
...................
Habari hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990














No comments:
Post a Comment