Na Magreth Kabyemela Dar es Salaam
...............................
SERIKALI ya Tanzania imetangaza kuwa mwenyeji wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (Regional Maritime University – RMU), hatua inayolenga kuimarisha elimu, utafiti na uzalishaji wa wataalamu katika sekta ya usafiri wa majini barani Afrika.
Taarifa hiyo imetolewa Oktoba 13, 2026, jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akieleza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOWCA) katika kufanikisha mpango huo.
Kihenzile amesema kuanzishwa kwa chuo hicho kutasaidia kuongeza upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi, kuimarisha tafiti na ubunifu, pamoja na kuwawezesha vijana kupata maarifa yatakayowaongezea nafasi za ajira katika sekta ya usafiri wa majini.
Amesema usafiri wa majini ni nguzo muhimu katika biashara ya kimataifa, huku Tanzania ikiwa na nafasi ya kimkakati kutokana na ukanda wake wa Bahari ya Hindi na ukaribu wake na nchi mbalimbali zisizo na mwambao wa bahari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.
Aidha, amesema maendeleo ya sekta hiyo yanahitaji uwekezaji katika miundombinu ya bandari, meli, teknolojia za kisasa, usalama wa majini na utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa. Hatua hizo zinaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa usafirishaji na ushindani wa bidhaa za Afrika katika masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Kusini na Kaskazini (MOWCA), Kassim Mpaata, amesema gharama za ujenzi wa chuo hicho zitagharamiwa kwa ushirikiano wa nchi wanachama, huku Serikali ya Tanzania ikiongoza mchakato huo.
Taarifa hiyo imetolewa kuelekea Mkutano wa 10 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la MOWCA, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuimarisha biashara na ushirikiano wa usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya maji.
Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Afrika kuzalisha wataalamu wake wa usafiri wa majini na kukuza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchukuzi.
Taarifa ikitolewa.










No comments:
Post a Comment