FCC YATWAA TUZO YA UBORA YA AFRIKA MASHARIKI 2026 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, November 5, 2026

FCC YATWAA TUZO YA UBORA YA AFRIKA MASHARIKI 2026

KIGALI, RWANDA – 2 NOVEMBA 2026.

Tume ya Ushindani (FCC) ya Tanzania imeibuka mshindi wa jumla katika kipengele cha Ubora wa Huduma kwa Taasisi za Umma katika Tuzo za Ubora za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Regional Quality Awards 2026), zilizofanyika usiku wa tarehe 2 Novemba 2026 katika Hoteli ya Movenpick jijini Kigali, nchini Rwanda.

Tuzo hiyo ni kutambua dhamira na juhudi za FCC katika kutoa huduma bora kwa Umma, kusimamia masoko kwa ufanisi, kulinda walaji na kuendeleza ushindani wa haki. Mafanikio hayo yanaifanya FCC kuwa miongoni mwa Taasisi za Umma zinazotambuliwa katika kuimarisha utamaduni wa ubora wa huduma ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

FCC imeshika nafasi ya kwanza katika kipengele hicho kupitia huduma zake za Usimamizi wa Masoko na Ushindani wa Haki, ikiibuka mshindi dhidi ya Taasisi nyingine zilizokuwa zimeingia katika kinyang’anyiro hicho kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taasisi hizo ni Kenya Electricity Generating Company PLC ya Kenya, iliyowasilisha huduma za uzalishaji wa umeme kwa kiwango kikubwa (Large-Scale Electricity Generation); Rwanda Meteorology Agency ya Rwanda, kupitia huduma za utabiri wa hali ya hewa (Weather Forecasting); pamoja na National Identification and Registration Authority (NIRA) ya Somalia, kupitia huduma za utambuzi wa utambulisho wa taifa (National Identification Services).

Kutambuliwa kwa FCC kunadhihirisha nafasi muhimu ya Tume katika kukuza mazingira ya soko yenye haki, uwazi na ushindani. Ubora katika soko hautegemei bidhaa na huduma zinazotolewa na wafanyabiashara pekee, bali pia uwepo wa ushindani wa haki, walaji wenye uelewa na mwenendo unaozingatia misingi bora ya biashara.

Tume ya Ushindani ilianzishwa mwaka 2003 na ina jukumu la kusimamia na kulinda misingi hiyo kupitia utekelezaji wa sheria za ushindani, ulinzi wa walaji, udhibiti wa miunganiko na ununuzi wa kampuni pamoja na udhibiti dhidi ya bidhaa bandia. Kupitia majukumu hayo, Tume inachangia kujenga mazingira ya biashara yanayoongeza imani ya walaji, kuchochea ubunifu na kuendeleza ukuaji endelevu wa uchumi.

Kuwezesha wananchi kupata huduma za udhibiti zilizo rahisi, zenye ufanisi na zinazozingatia mahitaji yao ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya FCC. Tume imeweka mifumo mbalimbali inayowawezesha walaji kuwasilisha malalamiko, wafanyabiashara kupata huduma za maombi ya kuunganisha kampuni na wadau kupata maelekezo pamoja na taarifa kuhusu masuala ya udhibiti wa ushindani na ulinzi wa walaji.

Aidha, FCC huendesha programu za uhamasishaji kwa Umma na ushirikishwaji wa wadau ili kuhakikisha walaji na wafanyabiashara wanafahamu haki zao, wajibu wao na matakwa ya sheria zinazohusu ushindani na ulinzi wa walaji. Uwepo wa ofisi za Tume katika maeneo mbalimbali nchini unaongeza fursa za kushirikiana na wananchi, wafanyabiashara na Taasisi au Mamlaka nyingine za udhibiti.

Katika kuimarisha ubora wa huduma, Tume imeendelea kuboresha mifumo yake ya utendaji kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Ubora unaozingatia viwango vya ISO 9001:2015, ambao iliupata mwezi Desemba 2024. Mfumo huo unalenga kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vinavyofanana, uwajibikaji unaimarishwa na maboresho yanafanyika kwa kuzingatia taratibu sanifu, ukaguzi wa ndani, maoni ya wadau na tathmini za mara kwa mara za menejimenti.

Vilevile, FCC inaendelea kutumia teknolojia za kidijitali ili kuongeza upatikanaji, ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma zake za udhibiti. Mfumo wa kielektroniki wa TANOGA unasaidia uratibu wa ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini na kuimarisha jitihada za kudhibiti bidhaa bandia, hatua inayochangia kulinda walaji na wafanyabiashara wanaofuata sheria.

Kupata tuzo hiyo ya heshima katika ngazi ya kikanda ni hatua muhimu katika safari ya maendeleo ya FCC. Zaidi ya kutambua mafanikio yaliyofikiwa, tuzo hiyo inaongeza wajibu wa Tume kuendelea kuboresha ubora, upatikanaji, ufanisi na mwitikio wa huduma zinazotolewa kwa Umma.

Katika kipindi kijacho, FCC itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu ya udhibiti, kupanua matumizi ya teknolojia za kidijitali, kuboresha ushirikishwaji wa wadau na kuongeza uelewa wa Umma kuhusu masuala ya ushindani na ulinzi wa walaji.

Tume pia itaendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kukuza matumizi ya taratibu bora za udhibiti, kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza katika masoko na kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao katika mazingira yenye ushindani wa haki.

Aidha, tuzo hiyo inakuwa chachu kwa FCC kuendelea kuinua viwango vya utendaji wa Taasisi, kuendeleza ubunifu na kuhakikisha manufaa ya huduma bora za Umma yanawafikia walaji, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla nchini Tanzania.

Kupitia jitihada hizo, FCC inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika ngazi ya kikanda kwa kuhakikisha huduma za udhibiti zinaendelea kuwa bora, zenye uwazi, zinazopatikana kwa urahisi na zinazozingatia mahitaji ya wananchi, huku ikiimarisha imani na matumaini ya Umma katika masoko ya Tanzania.

Tuzo za Ubora za Jumuiya ya Afrika Mashariki za mwaka 2026 ni mojawapo ya programu muhimu za Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazolenga kutambua mafanikio ya kipekee katika usimamizi wa ubora katika sekta za uzalishaji na utoaji wa huduma.

Tuzo hizo huwakutanisha na kutambua biashara pamoja na Taasisi za Umma zilizopendekezwa kupitia mashindano ya tuzo za ubora katika ngazi za kitaifa za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kupitia tuzo hizo, Taasisi na mashirika yanayodhihirisha dhamira ya kuzingatia ubora, ubunifu na maboresho endelevu hutambuliwa kwa mchango wake katika kuimarisha ushindani wa kikanda, ustahimilivu wa kiuchumi na ukuaji shirikishi.

Kupitia mpango huo, Sekretarieti ya EAC inalenga kuhamasisha matumizi ya viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa pamoja na mbinu bora za utendaji, kukuza ubunifu na maboresho endelevu na kuongeza uwezo wa biashara na Taasisi za Afrika Mashariki kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa hiyo, mafanikio ya FCC katika Tuzo za Ubora za EAC za mwaka 2026 si tu utambuzi wa mafanikio ya Taasisi ya Tanzania, bali pia ni mchango muhimu katika kutimiza dira ya kikanda ya kuimarisha ubora wa huduma kwa Umma, usimamizi madhubuti wa masoko na maendeleo endelevu ya uchumi.

Tume ya Ushindani inasisitiza dhamira yake ya kuendelea kuweka utoaji wa huduma bora kwa Umma kuwa kipaumbele cha kudumu, ili kuhakikisha utambuzi huu wa kikanda unatafsiriwa katika huduma bora zaidi, ulinzi imara wa walaji na mazingira ya soko yenye ushindani wa haki kwa manufaa ya wote.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad