Mkutano wa 48 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeanza leo, Novemba 23, 2026, katika eneo la Munyonyo, jijini Kampala, Uganda, ukilenga kupitia utekelezaji wa maamuzi na maagizo ya mikutano iliyopita pamoja na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na ushirikiano wa kikanda.
Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi na maagizo ya Baraza la Mawaziri lililopita, ripoti ya Katibu Mkuu wa EAC, pamoja na maendeleo ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, afya, usalama, siasa na sekta za uzalishaji.
Aidha, mkutano huo utapitia na kujadili hali ya kifedha na rasilimali watu katika Sekretarieti na Taasisi za Jumuiya, pamoja na kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Taasisi na Vyombo mbalimbali vya EAC. Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Afrika Mashariki (CASSOA), Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki (EACCA), Kamisheni ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (EAHRC), Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki (EASTECO), Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO).
Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku nane kuanzia Novemba 23 hadi 30, 2026, unafanyika kwa njia ya mseto (ana kwa ana na kwa njia ya mtandao), ambapo majadiliano yake yatafanyika katika ngazi tatu, ambazo ni; wataalamu kuanzia Novemba 23 hadi 26, Kamati ya Uratibu Novemba 28 na Baraza la Mawaziri Novemba 30, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Jamii na Siasa, Mhe. Andrea Aguer Ariik, amesisitiza umuhimu wa mkutano huo katika kutoa mwelekeo wa kisera na kusimamia utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo ya sekta mbalimbali katika Jumuiya.
Aidha, amewahimiza wajumbe kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kutoa mapendekezo yenye tija yatakayowezesha kufikiwa kwa maamuzi yanayochochea maendeleo ya kikanda na kukidhi matarajio ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Baraza la Mawaziri ni chombo kikuu cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kinachohusika na uundaji wa sera na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za Jumuiya. Baraza hilo linaundwa na Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na/au ushirikiano wa kikanda.
Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya wataalamu unaongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamin Mwesiga. Wengine katika ujumbe huo ni Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii, Mha. Adillah Mataka, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bi. Mwanamridu Amiry Jumaa, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Bw. Elisha Suku pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.











No comments:
Post a Comment